Katungwa aendelea kuhangaisha mabeki soka ya wanawake India

Katungwa aendelea kuhangaisha mabeki soka ya wanawake India

NA RUTH AREGE

STRAIKA wa Harambee Starlets Elizabeth Katungwa anaendelea kucheka na wavu Ligi Kuu ya Wanawake nchini India. 

Alifungia klabu yake ya Royal Rangers mabao mawili na kuifanya timu yake  kuandikisha ushindi wa 4-0 dhidi ya timu ya Eves.

Alifunga bao lake la kwanza katika dakika ya 18 na bao la pili alifunga dakika za lala salama kipindi cha pili. Kwa sasa Katungwa ana jumla ya mabao matatu kati ya mechi mbili ambazo amecheza msimu mpya.

Wiki iliyopita kwenye mechi ya kwanza ya ligi ya msimu wa 2022/23, alifunga bao moja. Kwenye mechi hiyo timu yake iliandikisha sare ya 2-2 dhidi ya klabu ya Delhi.

Msimu wa 2021/22, alikuwa miongoni mwa wafungaji bora na mabao 13. Katungwa anasema, lengo lake msimu huu ni kuwa mfungaji bora Ligi Kuu ya India.

“Najaribu sana timu yangu ichukwe ubigwa na pia niwe mfungaji bora ama niwe miongoni mwa wagungaji bora. Nina imani kwamba ninaweza. Kuwa kwangu hapa ni njia moja ya kuonyesha dunia nzima kuwa, Kenya kuna talanta za soka ya wanawake.”

“Nikiwa mchezaji wa kwanza kucheza nchini humu, najituma kila siku na sitachoka kupeperusha bendera ya taifa langu’” aliongezea Katungwa.

Kabla ya kujiunga na Rangers, alikuwa akiipigia klabu ya  Sethu FC ambayo aliiongoza kumaliza nafasi ya pili katika ligi kuu ya wanawake ya India msimu wa 2021/22 kwa alama 30. Timu ya Gokulam Kerala alishinda ligi wakiwa na pointi 33.

Baada ya kukamilika kwa ligi hiyo, Rangers, ambayo ni mojawapo ya klabu tajiri zaidi za kandanda za wanawake mjini New Delhi, India na inayoshiriki ligi ya daraja la kwanza, ilimsajili straika huyo wa Kenya kwa kandarasi ya miaka miwili.

Katungwa pia alitangazwa mshindi wa tuzo za Soya 2019 katika kitengo cha shule baada ya kuiongoza Kwale kupata ushindi maradufu katika soka ya wasichana kwenye fainali za shule za upili za kitaifa na Afrika Mashariki.

  • Tags

You can share this post!

Tumaini la wadau wa utalii liko kwa serikali

TAHARIRI: Sera mpya ya kifedha ya Ruto itaokoa raia wengi

T L