Makala

KAULI YA MATUNDURA: Furaha iliyoje kwamba sasa Uganda ina wataalamu wa Kiswahili zaidi ya mahitaji!

March 6th, 2019 2 min read

Na BITUGI MATUNDURA

TASWIRA dumifu (stereotype) kwamba ‘Kiswahili kilizaliwa Zanzibar, kikakulia Tanzania, kikaanza kuugulia Kenya, kikafia Uganda na kuzikwa Kongo’ inatoa taswira ya kuchangamsha na kuchekesha kuhusu lugha hii ya Kibantu – ambayo sikosei kudai kuwa ndiyo mojawapo ya lugha maarufu za Kiafrika ulimwenguni.

Maendeleo ya Kiswahili nchini Uganda kwa muda mrefu yalitatizwa na sera za kibwanyenye ambazo ziliisifu lugha hiyo kimdomo na kuikashifu kimoyomoyo.

Mumo kwa mumo katika sera hizo, lugha ya Luganda imekuwa ikileta ushindani mkubwa kwa Kiswahili.

Aidha, itikadi za kihistoria zilizoihusisha lugha ya Kiswahili na ‘dhuluma za kijeshi’ zimeanza kuyeyuka – na hivyo basi Uganda kuanza kukikumbatia Kiswahili.

Kulingana na utafiti uliofanywa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki (KAKAMA), takriban taasisi 18 vikiwemo vyuo vikuu nchini Uganda, zinafundisha Kiswahili.

Katibu Mkuu wa KAKAMA, Prof Kenneth Inyani Simala asema kwamba kuna uwezekano Uganda ina walimu wengi wa Kiswahili hivi kwamba nchi hiyo inaweza kuwatuma walimu hao nje katika mataifa mengine ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kufundisha Kiswahili.

“Mwisho wa Machi 2019 KAKAMA inatarajia kuwasilisha rasmi ripoti ya Utafiti huo,” Prof Simala akaambia Taifa Leo.

Alisema kwamba, kila mwaka, zaidi ya vyuo vikuu vinne nchini Uganda huwa na wanafunzi wanaofuzu kutoka kwa taasisi hizo baada ya kusoma Kiswahili.

Licha ya hatua hiyo ya kutia moyo, Prof Simala asema kwamba tatizo kubwa ni kuwa somo la Kiswahili si la lazima nchini humo na hivyo basi kuchangia katika shule chache kutolifundisha.

Walimu

Mtaalamu huyu pia alidokeza kwamba walimu wa Kiswahili nchini Uganda hulipwa mshahara wa kiwango cha chini wanapolinganishwa na wenzao waliosomea masomo ya sayansi – hali inayochangia walimu hao ‘kutokomea’.

Vyuo vikuu vinavyofundisha Kiswahili nchini Uganda ni pamoja na Kyambogo, Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Uganda, Makerere, Bishop Steward miongoni mwa vingine.

Katika kipindi cha miaka miwili hivi iliyopita, Afrika Mashariki imekwisha kushuhudia mwamko mpya katika masuala yanayohusu maendeleo ya Kiswahili.

Kwa hivi sasa, kuna mikakati ya kuhakikisha kwamba kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inabuni Baraza la Kiswahili. Asasi hii itapiga jeki michakato ya kukistawisha Kiswahili kimakusudi.

Kiswahili kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni 120 kote ulimwenguni – wengi wao wakiwa ni wenyeji wa Afrika ya Mashariki na mataifa ya Maziwa Makuu. Vyuo vikuu nchini Marekani na Barani Ulaya vinafundisha Kiswahili.

Kutokana na umaarufu wa Kiswahili – wataalamu wanaelekea kukubaliana kwamba lugha hii ina uwezo wa kuwa lingua franca ya bara la Afrika.

Ni matarajio yangu kwamba mwamko huu mpya nchini Uganda utatiliwa mbolea ili Kiswahili kiendelee kunawiri.

 

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]