Makala

KAULI YA MATUNDURA: Huu ndio mtazamo wa mwandishi Ayi Kwei Armah kuhusu sanaa ya uandishi wa kubuni

May 22nd, 2019 2 min read

Na BITUGI MATUNDURA

MNAMO Januari 2005 nilihudhuria mhadhara wa mwandishi Ayi Kwei Armah wa Ghana kwenye ukumbi wa Taifa Hall, Chuo Kikuu cha Nairobi.

Katika kipindi hicho, raghba yangu ya kutaka kuwa mwandishi ilikuwa katika upeo wake.

Riwaya yangu – Mkasa wa Shujaa Liyongo ilikuwa imekwisha kuchapishwa na Phoenix Publishers Limited – baada ya vuta n’kuvute kali ambayo mara nyingi huwakatisha tamaa waandishi chipukizi.

Nisingalikuwa na moyo wa chuma kipindi hicho, labda ningaliachana kabisa na uandishi.

Lakini ninapovuta taswira kuhusu safari yangu ya uandishi, ninahisi kwamba kamwe sina majuto.

Yaliyonisibu labda ni kisa nitakachokisimulia wakati mwingine. Kwa hiyo, malengo ya kuhudhuria mhadhara wa mwandishi huyu yalikuwa ni mawili.

Kwanza, nilitaka kusikia tajriba yake na mtazamo wake kuhusu sanaa na fani ya uandishi.

Pili, nilitaka kukutana na mwandishi mwenyewe baada ya kusoma tungo zake kama vile The Beautiful Ones Are Not Yet Born (1968), Two Thousand Seasons (1973), The Healers (1973) na Why Are We So Blest? (1973).

Kazi nyingi za mwandishi huyu ziliwahi kuorodheshwa katika msururu wa tungo za African Writers Series (AWS) – ambao kwa yakini ulionesha nani ndiye nani katika uandishi wa fasihi ya Kiafrika punde tu baada ya mataifa mengi ya bara hili kujinyakulia uhuru.

Saa nane juu ya alama, ukumbi wa Taifa Hall, chuoni Nairobi ulikuwa umejaa pomoni.

Wahadhiri, wanahabari na wanafunzi walikuwa wameketi tayari kumsikiliza Ayi Kwei Armah. Mhadhara wake ulitamba kwenye mawanda mapana kuhusu historia na mahusiano ya Afrika, utamaduni wake na ukoloni.

Alidai kwamba katika mtagusano wa watawala wa kikoloni na Waafrika, wakoloni waliwadhalilisha Waafrika kwa namna ambayo iliwafanya wadharau tamaduni zao.

Alidai kwamba mpaka sasa, dhana ya uhuru wa Mwafrika ni dhana ya kimzaha tu.

Alisisitiza kwamba uhuru wa kisiasa kamwe hauwezi kuwa na manufaa ikiwa Waafrika hawatakuwa na uhuru wa utamaduni wao. Mwandishi huyu alizungumzia kuhusu mikabala mine ambayo inaweza kumfaa zaidi mwandishi yeyote – hasa mwanndishi chipukizi (kama mimi wakati huo) katika kuandika tungo za ‘masafa marefu’.

Kwanza, alisema kuwa uandishi ni sanaa ambayo inahitaji kukabiliwa na ufundi wa namna fulani.

Pili, alishauri kwamba sharti mwandishi awe na raghba (inspiration) ya kutaka kuandika.

Tatu, alisema kwamba lazima mwandishi awe mtu makini na anayefanya kazi kwa bidii. Alikariri kwamba mwandishi mara nyingi ni mtu mwenye ukiwa kwa sababu ndiyo kawaida ya kuandika.

‘Sisi wenyewe’

Aliendelea kusema kwamba matatizo ya bara la Afrika yana suluhisho mumo kwa mumo katika bara hili – kwamba hatuwezi kutarajia suluhisho kutoka popote isipokuwa Afrika.

Mwisho, mwandishi huyu aligusia suala nyeti kuhusu lugha inayopaswa kutumika kutungia fasihi ya Afrika.

Mhadhara ule ulipomalizika, kipindi cha maswali kilijiri. Niliuinua mkono wangu kutaka kumuuliza swali kuhusu nafasi ya Kiswahili katika uanndishi wa fasihi ya Kiafrika – na mstakabali wa lugha yenyewe katika ulingo wa kimataifa pamona na usemezano wa utamaduni wa Mwafrika na staarabu nyingine ulimwenguni.

Kwa bahati mbaya, mkono wangu ulipotelea kwenye ‘misitu ya mikono’ mingine iliyoinuliwa na watu wengine waliotaka kuuliza maswali.

Liwe liwalo, nilijifunza kutoka kwa mwandishi Ayi Kwei Armah kwamba uandishi ni taaluma inayohitaji subira na uvumilivu.

Ikiwa mtu hana hulka ya kudumisha mambo haya mawili, nafikiri ni muhimu ‘ ajipe shughuli’ ya kufanya mambo mengine tofauti.

Vinginevyo, atavunjika moyo bure bilashi.

[email protected]