KAULI YA MATUNDURA: Kiswahili ni ufunguo wa milango ya masoko ya Afrika Mashariki kwa mataifa mengi ya Magharibi

KAULI YA MATUNDURA: Kiswahili ni ufunguo wa milango ya masoko ya Afrika Mashariki kwa mataifa mengi ya Magharibi

NA BITUGI MATUNDURA

KATIKA makala yangu juma lililopita, niliuliza maswali mawili ya balagha.

Je, ni kwa nini nchi za kigeni kama vile Japan, Marekani, Uchina na Uingereza zinawekeza kimakusudi katika taasisi zao za mafunzo ili watu wao wajifunze Kiswahili? Je, ni kwa sababu Kiswahili Kinapendwa?

Maswali haya yalichochewa na kutuzwa kwa mwalimu, mwandishi, mhariri na mfasiri – Bw Ali Attas na nchi ya Japan, kwa mchango wake wa kuwa balozi wa lugha na utamaduni wa Kiswahili nchini humo.

Kwa ‘bahati mbaya’ – nafikiri kwa maksudi, tuzo aliyokabidhiwa Bw Attas iliandikwa kwa Kijapani. Lugha zote duniani, hususan lugha kuu zimeanza kuchukuliwa kuwa raslimali kuu.

Lugha zenye wasemaji wengi na ushawishi mkubwa zimebidhaaishwa, mbali na kutumika kama nyenzo kuu za kufanikisha maslahi ya kibiashara katika pembe mbalimbali za ulimwengu.

Kiswahili kwa mfano kinazungumzwa na takriban zaidi ya watu milioni 250 kote duniani. Wasemaji wengi ni watu wa Afrika ya Mashariki na nchi za Maziwa Makuu.

Lugha hii, mbali na kuwa kitambulisho cha utamaduni wa eneo hili, ndiyo Lingua Franka ya Afrika Mashariki. Kutokana na umuhimu wake, tayari Kiswahili kimepigiwa kura kuwa lugha ya mawasiliano mapana barani Afrika.

Umaarufu wa Kiswahili hivyo basi umechangia katika mataifa ya kimagharibi kuitambua kuwa ndiyo ufunguo utakaoyawezesha kufungua milango ya masoko ya Afrika ya Mashariki.

Kampuni kuu za kimataifa kama Microsoft zimefanya juhudi za kimakusudi kuingiza Kiswahili katika mifumo ya kompyuta. Hii ni hatua kuu na ya kutia moyo.

  • Tags

You can share this post!

Didmus Barasa asema anayefaa kukamatwa ni Raila

Serikali ya Lamu lawamani kwa kulipa wafanyakazi hewa...

T L