Makala

KAULI YA MATUNDURA: Maneno ‘benki’na ‘banki’ hayakufaa kuibua mitanziko yoyote, yote mamoja

June 26th, 2019 2 min read

Na BITUGI MATUNDURA

MNAMO 2010, Kampuni ya Uchapishaji wa Vitabu – Longhorn Publishers Limited, Nairobi – ilinishirikisha katika mradi wa uandaaji wa Kamusi ya Karne ya 21.

Shughuli hii ilinikutanisha na wanaleksikografia wapevu wa Kiswahili Afrika ya Mashariki kama vile Maprofesa James Salehe Mdee na John Gongwe Kiango.

Kadhalika nilikutana na mwanaistilahi Makih Hassan kutoka Baraza La Kiswahili la Tanzania; BAKITA.

Shughuli hiyo ilinifundisha mambo mengi kuhusu mchakato wa uundaji wa kamusi; hasa uteuzi, uingizaji na utomeshaji wa vidahizo katika kamusi ya kawaida.

Hata hivyo, funzo kuu nililopata ambalo linahusiana na kauli ya makala yangu hivi leo ni kwamba lugha yoyote iwayo ni kwamba uundaji wa kamusi ni shughuli ambayo haina kikomo.

Kwa nini? Kwa sababu lugha ni kitu kilicho hai, kinakua na kuwa kila uchao, kinabadilika na wakati mwingine kufa.

Hii ina maana kwamba, ikiwa Kamusi ya Karne ya 21 imekwenda kwenye matbaa (press) leo, wanaleksikografia huanza kuihariri tena kesho yake ili kubaini iwapo kuna neno lililoachwa nje au kuna neno jipya lililozuka ambalo linapaswa kuingizwa na kutomeshwa kamusini.

Kimsingi, uandaaji wa kamusi ni shughuli ambayo haiwezi kutamatika na kwamba haiyumkiniki kamusi moja kukusanya maneno yote katika lugha yoyote iwayo.

Hulka ya lugha ni kwamba, hata neno ambalo halikufaulu kuingizwa katika kamusi mwaka huu huenda likaingizwa katika siku au miaka ya baadaye kwa sababu watumiaji wa lugha ndio wenye usemi mkubwa na wanahusa na wadau wakuu katika masuala yoyote yanayohusu lugha yao.

Matamshi na tahajia

Mkabala huu unanirejesha kwenye mdahalo wa hivi majuzi kuhusu msamiati ‘Banki’ na ‘Benki’.

Noti za sarafu ya Kenya zimeandikwa ‘Banki Kuu ya Kenya’ ilhali zile za Tanzania zimeandikwa ‘Benki Kuu ya Kenya’.

Kwa hiyo, watu ambao hawana ujuzi wa lugha walitanzika kuhusu hali hii. Neno Banki/Benki limetoholewa kutokana na neno la Kiingereza ‘Bank’ ambalo linatamkwa /benk/.

Kwa hiyo, Tanzania inapoandika kwenye sarafu yake ‘Benki Kuu ya Tanzania’ bila shaka imezingatia matamshi zaidi na kupuuzilia mbali hijai au maendeleo.

Aidha, Kenya inapoandika kwenye noti zake: ‘Banki Kuu ya Kenya’ imezingatia zaidi hijai (mwendelezo) kuliko matamshi.

Kamusi yoyote nzuri itayatomesha maneno haya kuwa ni visawe.

Mdahalo kuhusu ‘Banki’ nchini Kenya na ‘Benki’ nchini Tanzania ulipozuka, mimi sikuona sababu yoyote ya kujadili suala hilo.

Hata hivyo, mdahalo huo ungekuwa wenye mashiko mno ikiwa baadhi ya noti nchingi Kenya zingekuwa zimeandikwa ‘Banki’ na ‘Benki’ au za Tanzania kuandikwa ‘Benki’ na ‘Banki’ kwa sawia.

Hii ina maana kwamba, ikiwa nchi imeamua kutumia mkabala wa hijai, haiwezi kutumia mkabala wa matamshi kwa wakati mmoja.

Vivyo hivyo, halitakuwa kosa kwa Kenya kuandika ‘Benki’ kwenye noti zake miaka ijayo – wala haitakuwa kosa kwa Tanzania kutumia ‘Banki’ kwenye noti zake.

Ikumbukwe kwamba ingawa Kiswahili ni lugha sambazi Afrika ya Mashariki, hatuwezi kuufumbia macho ukweli kwamba kuna ‘Kiswahili cha Kenya’ na ‘Kiswahili cha Tanzania’ kwa sababu ya suala linalojulikana kama ‘lahaja za kijiografia’ (georaphical dialects).

Maelezo aliyotoa Gavana wa Benki Kuu, Dkt Patrick Njoroge kwamba Kenya inatumia neno ‘Banki’ kwa sababu ati lilipendekezwa na Tom Mboya si ya kitaalamu.

 

Bitugi Matundura ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka

[email protected]