Makala

KAULI YA MATUNDURA: Matumizi ya Kiswahili na wageni si kigezo faafu cha kupima thamani ya lugha hiyo

July 17th, 2019 2 min read

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA gazeti la Daily Nation toleo la Julai 11, 2019, kulikuwa na habari kwamba mwanamuziki, mtunzi wa nyimbo na mwigizaji wa Marekani Beyonce Giselle Knowles-Carter alitumia maneno ya lugha ya Kiswahili katika wimbo wake mpya.

Maneno ya Kiswahili yanayosikika katika wimbo huo ni “Uishi kwa muda mrefu mfalme.”

Tukio hili aghalabu lilizua msisimko wa namna fulani miongoni mwa wakereketwa wa Kiswahili Afrika ya Mashariki.

Wakati huo huo, mtaalamu Prof Aldin Kai Mtembei alizua mdahalo katika ukumbi wa WhatsApp wa wanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) alipotuma kauli iliyojaa kejeli na tashtiti kuhusu aina moja ya mvinyo uliotengenezwa nchini ujerumani. “Jinsi Kiswahili kinavyochanja mbuga: Bia imetengenezwa Ujerumani, inauzwa China – na katika melezo yake kuna pia Kiswahili.

Mojawapo ya maelezo katika bia hiyo – Original German Black Beer – Oettinger Schwarz, kuna onyo lililoandikwa kwa Kiswahili – “Unywaji wa pombe kupita kiasi unaweza kudhuru afya yako. Usiuzie yeyote aliye chini ya umri wa miaka 18. Kunywa pombe kiungwana”.

Mtaalamu Melkiory Fursa aliuliza: Kwa nini walitumia lugha ya Kiswahili? Ni kwa kuwa kinapendwa (Ujerumani)? Wanywaji ni Waswahili na si wazungu? Waswahili hupenda kulewa? Au lugha ya Kiswahili ina mvuto kibiashara?”

Mtaalamu huyu alihisi kwamba Isimujamii ilihitajika mno ili kujibu maswali aliyoyauliza.

Matukio haya mawili – muziki wa Beyonce wenye maneno ya Kiswahili na pombe ya Ujerumani yenye onyo lililoandikwa kwa Kiswahili yanapaswa kutuchochea kutafakari upya kuhusu uzalendo wetu katika kuzikumbatia na kuzienzi lugha zetu za Afrika – hususan Kiswahili.

Mimi nilihisi kwamba hatua ya bia ya Ujerumani kusheheni maandishi ya Kiswahili ni mbinu ya kupanua soko la pombe hiyo.

Upokeaji

Bara la Afrika linapokea na kutumia bidhaa nyingi kutoka nje ikilinganishwa na bidhaa kutoka Afrika zinazouzwa katika maeneo mengine ulimwenguni. Ninahisi kwamba hakuna cha kusherehekea kwamba Kiswahili kimetambuliwa na wazungu. Mbona sisi tusizitambue na kuzienzi lugha zetu – wazungu wawepo au wasiwepo?

Je, wazungu ndio kigezo cha utambuzi wa lugha na tamaduni zetu? Je, vikadiria viwango (rating scale) vya ufanisi wa lugha za Waafrika ni utambuzi wa lugha zenyewe na wazungu?

Nimewahi kudai kwamba ikiwa kuna raslimali kuu ambayo Afrika ya Mashariki inamiliki – basi ni Kiswahili. Kiswahili kinaweza kubidhaishwa na kuuzwa katika mataifa ya kigeni nje ya bara hili kwa namna inayoweza kuziletea nchi za Afrika ya Mashariki mapato makubwa.

Tusidanganyike kwamba Wazungu wanakichangamkia Kiswahili kwa sababu wanakipenda. Mumo kwa mumo katika kukichangamkia Kiswahili kuna maslahi ya kibinafsi.

Kampuni za kimataifa kama vile Microsoft zinapotumia Kiswahili katika mtandao wa intaneti, maslahi yao ya kibiashara ndiyo yamepewa kipaumbele.

Inasadifu tu kwamba katika kuafikia maslahi hayo, wanakitandawazisha Kiswahili bila wao kujua.

Juhudi hizi hazipaswi kupingwa – bali kuungwa mkono. Kilichoko ni Waafrika kujifungata masombo kujikomboa kutokana na kasumba za kikoloni ambazo zilichangia mno katika kuwafanya Waafrika kuzionea aibu lugha na tamaduni zao.

[email protected]