Makala

KAULI YA MATUNDURA: Mbinu za upanuzi wa leksikoni katika lugha ya Kiswahili na changamoto zake

September 18th, 2019 2 min read

Na BITUGI MATUNDURA

KATIKA kipindi cha majuma mawili yaliyopita, makala yangu yamejikita katika uwanja wa leksikolojia.

Leksikolojia ni taaluma ambayo hujishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na uchanganuzi wa msamiati wa lugha pamoja na maana zake.

Uwanja huu vilevile huitwa elimumsamiati. Istilahi ni msamiati katika nyanja maalum za lugha kama vile sheria, tiba, teknohama, biolojia, fizikia, kemia na kadhalika.

Mpaka baina ya msamiati na istilahi ni mwembamba mno kwa msingi kwamba, istilahi inapobuniwa katika lugha fulani na ikawa inakubaliwa na kutumiwa, inakuwa ni msamiati wa ile lugha.

Kwa hiyo, istilahi ni msamiati wa lugha katika uwanja maalum.

Msururu wa makala haya ulichochewa na juhudi za mwandishi na mwanahabari, Bw Geoffrey Mung’ou aliyependekeza istilahi ‘runulishi’ kwa maana ya smartphone. Bw Mung’ou alitumia mchakato wa uhulutishaji wa maneno mawili ‘rununu’ na ‘tarakilishi’ ili kubuni ‘runulishi’.

Mkabala huu umewahi kutumiwa na wataalamu wengine kama vile Prof Rocha Chimerah kubuni maneno kama ‘tarakilishi’. (Hata hivyo, mimi nimekwisha kupendekeza kwamba mtaalamu huyu aifanyie marekebisho istilahi yake ili iwe ‘rununulishi’. Nimekwisha kutoa sababu za kumtaka Bw Mung’ou airekebishe istilahi yake iwe ‘rununulishi’ badala ya ‘runulishi’.

Kiingereza nilivyokwisha kutaja katika makala ya awali ni lugha inayopanua leksikoni yake kwa kuegemea Kigiriki, Kilatini na lugha nyingine kuu ulimwenguni. Lugha hizi zinategemea unominishaji zaidi kuliko uambishaji – unaoonekana zaidi katika lugha za Kibantu.

Nadharia ya Mzee Sheikh Ahmad Nabhany kuhusu upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili ni kwamba lahaja za Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika – hususan lugha za Kibantu ni kanzi muhimu ya kuanzia pale tunapotafuta dhana au neno la kuiita dhana ngeni.

Pale ambapo dhana hiyo inakosa kabisa, Mzee Nabhany anapendekeza kwamba neno au istilahi ibuniwe kwa kuangalia mambo matatu; Kwanza ni muhimu kuangalia umbo la kitu.

Pili, zingatia utenda kazi wa kitu. Tatu, ni muhimu kuzingatia sauti au mlio wa kitu.

Kwa hiyo, tukiirejelea istilahi ya ‘runulishi’ aliyopendekeza Bw Mung’ou, tunagundua kwamba inajikita katika nadharia ya Mzee Nabhany – ambapo muundaji amezingatia utendakazi wa kifaa.

Kwanza, jinsi tulivyokwisha kusema, ‘smartphone’ ni simu (rununu na vilevile inaweza kutenda kazi ileile ya kompyuta au tarakilishi. Kwa mantiki hii, Bw Mung’ou amehulutisha maneno ‘rununu + tarakilishi’ ili kupata ‘runulishi’. Ili kuiepusha istilahi hii (runulishi) na ugiligili na ugumu wa kuitamka, ninapendekeza kwamba iwe ‘rununulishi’.

Je, ‘smart –Tv’ tutaiitaje? Tatizo hili linaturudisha kwenye miundo tofauti ya lugha za Kiingereza na Kiswahili hasa katika suala zima la upanuzi wa leksikoni ya Kiswahili.

Jambo la kutia moyo ni kwamba, katika ufinyu wake wa kutumia neno moja kurejelea aina mbalimbali za dhana ambazo zimekurubiana, Kiswahili huenda kisihitaji sana au kwa dharura istilahi ya ‘Smart TV’ au hata ‘smartphone’ kwa msingi kwamba dhana televisheni na rununu/ au simu zinaeleweka vizuri pale zinapotumiwa na wasemaji wa Kiswahili. Jambo lililo muhimu ni kwamba, midahalo ya aina hii inakuza Kiswahili kinadharia hata pale ambapo suluhisho la kiutendaji huenda lisipatikane.

 

[email protected]