Makala

KAULI YA MATUNDURA: Mradi wa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia masomo yote umefikia wapi?

March 8th, 2018 2 min read

Na BITUNGI MATUNDURA

MIAKA kumi na mitano hivi imepita tangu mdahalo mkali ulipoibuka baina ya wataalamu wa lugha kuhusu ufaafu wa matumizi ya Kiswahili katika ufundishaji wa masomo yote yakiwemo ya sayansi katika asasi za elimu Afrika Mashariki.

Watafiti wa lugha wamekuwa wakikipigia upatu Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia masomo yote isipokuwa yale ya lugha za kigeni katika shule za msingi na upili.

Kwenye kikao cha wataalamu wa Kiswahili kilichofanyika mapema 2003, wanachama wa Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (Chakama) waliazimia kuanzisha shule za kimajaribio – ya msingi ya ya upili kutumiwa kutekeleza mradi huo.

Kwenye kikao hicho, iliazimiwa kwamba Kenya na Uganda zianzishe kila moja shule za majaribio katika utumiaji wa Kiswahili katika kufundishia masomo yote; nayo Tanzania ianzishe shule ya upili kutekeleza mradi huo.

Hivyo basi Chakama kiliteua kamati ya wanakamati watano kuchunguza mpango wa utekelezaji wa mradi huo.

Kamati hiyo iliwahusisha Prof Kimani wa Njogu ambaye ni mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Kiswahili cha Taifa, Chakita- Kenya, Dkt Issa Ziddy wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Prof Austin Lwanga Bukenya wa Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda na Maprofesa Mugyabuso Mulinzi Mulokozi na Fikeni Senkoro wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wanataaluma hao walisema lugha ya Kiswahili ilikuwa inakua na kuenea haraka katika mataifa ya Maziwa Makuu hususan Rwanda, Burundi na Kongo-Brazzaville, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Msumbiji na Zambia.

Walisema kuwa Afrika Mashariki inapaswa kuwa kwenye msitari wa mbele katika shughuli za utafiti na kufanikisha azma ya matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika taasisi za elimu.

 

Mgawanyiko

Hata hivyo, azimio la kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia lilizua mgawanyiko mkubwa baina ya wataalamu wa Kiswahili – mgawanyiko ambao naamini ungalipo hadi wa leo.

Dkt Casmir Lubagumya, mhadhiri mkuu katika Idara ya Isimu na Lugha za Kigeni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema, haikuwa vyema wanataaluma wanaounga mkono matumizi ya Kiswahili katika kufundishia kuchukulia kwamba Kiswahili ni lugha ya kwanza au lugha mama kwa wanafunzi wote wa shule za msingi na upili Afrika Mashariki, au kuchukulia kwamba wanafunzi wote katika viwango hivyo ni weledi wa Kiswahili.

Alisema, nchini Tanzania ambapo Kiswahili kimekubalika na kusambaa sana, ni asilimia 10 pekee ya watu wanaokizungumza Kiswahili kama lugha yao ya kwanza.

Mbali na hayo, mdahalo kuhusu matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia ulipanda na kufikia viwango vya juu pale ambapo baadhi ya wataalamu walihoji ubora wa kuitumia lugha hiyo kufanya hivyo.

Isitoshe wanataaluma wengine walidai kwamba kuna istilahi chache mno za kuelezea dhana sa kisayansi mbali na kutokuwepo kwa vitabu vya kiada kutumiwa katika mtaala huo.

Mantiki ya uamuzi wa kutumia Kiswahili kufundishia inatokana na ukweli kwamba, kuna mataifa ambayo yametegemea lugha zao kupiga hatua kubwa kisayansi na kiteknolojia.

Inaaminika kwamba, kuna maarifa ya kiasili ambayo yamefumbatwa tu na lugha zetu za kiasili na hayawezi kwa vyovyote kuelezwa au kufafanuliwa kwa lugha nyingine za kigeni. Baadhi ya mataifa yanayosukuma mbele ajenda ya kutegemea lugha zao kufundishia na uvushaji wa maarifa ni pamoja na Japan na Uchina.

Na kwa hakika mataifa haya yamevunjilia mbali imani kwamba ni lazima utegemee lugha za kigeni kama vile Kiingereza – tunavyofanya hivi sasa kupiga hatua kubwa katika maendeleo.