KAULI YA MATUNDURA: Mshabaha kati ya Rais Magufuli na Kinjeketile Ngwale wa mwanatamthilia Ebrahim Hussein

KAULI YA MATUNDURA: Mshabaha kati ya Rais Magufuli na Kinjeketile Ngwale wa mwanatamthilia Ebrahim Hussein

Na BITUGI MATUNDURA

HAIWEZEKANI kamwe kushiriki diskosi ya siasa za Afrika ya Mashariki katika siku za hivi punde bila angalau kulitaja jina la rais wa Tanzania – Dkt John Pombe Joseph Magufuli aliyefariki hivi majuzi.

Ninachukua fursa hii kutoa risala zangu za rambirambi kwa raia wa Tanzania kwa kumpoteza rais wao. Kifo cha rais John Magufuli ni pigo kubwa si tu kwa nchi yake – bali pia Afrika ya Mashariki na Kati, maeneo ya Maziwa Makuu na bara zima la Afrika kwa jumla.

Mauko ya rais huyu na hususan mkabala na sera zake za kuukemea ubeberu, ufisadi na vita dhidi ya maradhi hatari ya korona vinanichochea kumlinganisha na mhusika – Kinjeketile Ngwale katika tamthilia maarufu ya Kinjeketile (Ebrahim Hussein, Oxford University Press -1969).

Tamthilia ya Kinjeketile imesukwa na kukitwa kwenye kiunzi cha Kinjeketile wa kihistoria aliyewaongoza Watanganyika katika Vita vya Maji Maji (1904 -1905).

Kwa kuwa fasihi mara nyingi huakisi na kufumbata tajriba na matukio halisi katika maisha ya binadabu, sikosei kudai kwamba si ajabu hulka na sifa za Kinjeketile Ngwale kujitokeza katika rais wa Tanzania – John Pombe Magufuli.

Katika tamthilia ya Kinjeketile, Ebrahim Hussein anasema kwamba Mjerumani alipofika Tanganyika, aliwaamrisha Wamatumbi kulipa kodi. Isitoshe Watanganyika walikabiliwa na dhiki nyingine kama vile njaa, maonevu na kupigwa. Katika hali hiyo, akajitokeza ‘mkombozi’ wao – Kinjeketile aliyeishi kijiji cha Ngarambe karibu na kijito cha Mto Rufiji. Kinjeketile alipandwa na pepo aliyekuwa akiishi katika bwawa hilo.

Akawafundisha Waafrika maana ya umoja, akawatia moyo kwa kuibuka na dhana ya maji. Waafrika wakawa na umoja na nguvu. Watu wengi waliosikia jina lake kwa njia ya ‘nywiywila’ wakaja kumuunga mkono. Maji haya kulingana na matamshi yake yangewazuia watu wasidhuriwe na risasi za Wajerumani ambao waliikalia nchi yao kwa mabavu.

Vivyo hivyo, rais John Pombe Magufuli alikuwa ‘mkombozi’ wa wanyonge na maskini kutokana na ufisadi. Katika kipindi cha miaka sita alichoiongoza Tanzania, alijaribu kadri ya uwezo wake kuwawezesha Watanzania wengi kiuchumi. Katika kipindi hicho, alibadilisha pakubwa amara au miundombinu ya Tanzania. Sawa na Kinjeketile, rais Magufuli alikuwa aliwaelekeza Watanzania katika mkondo wa imani ya maombi kwa Mwenyezi Mungu.

Aliamini kwamba sala ingekuwa silaha kuu katika kukabiliana na ugonjwa wa korona ambao umeutikisa ulimwengu. Akapuuza masharti ya sayansi kama vile kuvaa barakoa na kujiepusha na misongamano na kubanana kwa watu. Akapendekeza kuwa watu wajivukizie.

Mshabaha mwingine kati ya Kinjeketile na rais Magufuli ni kwamba wote wawili walipata ufuasi mkubwa. Jinsi ambavyo dhana ya maji ilivyoteka akili za Watanganyika katika Kinjeketile, ndivyo dhana ya maombi ilivyowateka bakunja raia wengi wa Tanzania. Hata katika hafla ya maombolezo yake, hatukuona raia wengi wa Tanzania wakiwa wamevalia barakoa. Kilele cha tamthilia ya Hussein – Kinjeketile ni kwamba Wamatumbi, Wapogoro, Wazaramo, Wakichi na watu wote wanayaamini ‘dhima ya maji kijinga’ na wanafyekwa na risasi za Mjerumani. Kinjeketile anatiwa mbaroni na kukataa kukana kuwa maji ni uwongo hata baada ya kupigwa mno. Anasema mwishoni mwa mchezo, “Neno limezaliwa […].

Siku moja neno hilo halitakuwa ndoto, bali ukweli. Sawa na Kinjeketile, rais Magufuli amekwisha kufariki. Maneno na azma yake kuhusu Tanzania na bara la Afrika na uhuru wa Mwafrika yatakuwa ya kweli siku moja.

mwagechure@gmail.com

You can share this post!

Maelfu katika hatari ya kufa kwa corona

SAUTI YA MKEREKETWA: Pumzika kwa amani Jemedari Magufuli