Makala

KAULI YA MATUNDURA: Ni pigo kwa ulimwengu wa Kiswahili kumpoteza Prof Mwenda Mukuthuria

August 1st, 2018 2 min read

Na BITUGI MATUNDURA

Mhariri. Naomba unipe idhini niitumie safu hii kumuomboleza mwalimu na rafiki yangu Prof Mwenda Mukuthuria  (pichani anayepokezwa mikrofoni) ambaye alitutupa mkono Jumamosi, juma lililopita. Jumamosi ambayo ni ya mkosi.

Maombolezo haya pia ni kwa niaba ya wanataaluma wengine wa Kiswahili ambao waliwahi kutangamana na kutagusana na Prof Mukuthuria, ambaye hadi mauko yake alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara, Narok.

Mara yangu ya kwanza kukutana na Prof Mukuthuria ilikuwa ni mwaka 2001 katika kongamano la ‘Lugha na Utandawazi’ mjini Nyahururu. Kongamano hilo liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Laikipia na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA).

Mwaka mmoja baadaye, tulikutana naye tena katika kongamano la Kiswahili mjini Arusha, Tanzania ambapo Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki – CHAKAMA kilizinduliwa.

Urafiki tuliouanzisha Nyahururu uliota mizizi na kushamiri. Katika kipindi hicho, alikuwa mhadhiri katika Chuo cha Kiisilamu cha Uganda.

Mnamo 2010, ujaala ulitukutanisha tena nilipokwenda kutafuta ajira katika Chuo Kikuu cha Chuka ambapo tulihudumu pamoja kwa miaka mitatu kabla hajaguria Chuo Kikuu cha Mount Kenya ambapo alikwezwa hadhi na kuwa Profesa Mshiriki wa Kiswahili.

Baada ya kuhudumu katika chuo hicho kwa muda, Prof Mukuthuria alihamia Chuo Kikuu cha Maasai Mara ambapo alihudumu wadhifa wa Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Fani.

Wataalamu mbalimbali wa Kiswahili walipokea taarifa kuhusu kifo cha Prof Mukuthuria mnamo Jumamosi 28, 2018 kwa masikitiko makubwa. Prof Kimani Njogu – mwenyekiti mwasisi wa CHAKITA alimtaja Prof Mukuthuria kuwa msomi mwadilifu, mwaminifu na mtu wa kutegemewa.

Prof Mukuthuria aliwahi kuwa mhazini wa Chama cha Kiswahili cha Taifa – ambacho ni chombo kilicho katika msitari wa mbele kutetea makuzi ya Kiswahili nchini Kenya.

Wataalamu wengine walioomboleza mauko ya Prof Mukuthuria ni pamoja na Dkt Mark Kandagor (Mwenyekiti, CHAKITA), Prof Clara Momanyi, Prof Kineene wa Mutiso (Nairobi), Prof Chacha Nyaigotti Chacha , Prof John Kobia (Chuo Kikuu cha Chuka), Prof Ken Walibora, Prof Sangai Mohochi (Chuo Kikuu Rongo). Wengine ni Prof Obuchi Moseti (Moi) Prof Ipara Odeo miongoni mwa wengine. Marehemu Prof Mwenda Mukuthuria alizaliwa katika kijiji cha Mwigele, Kata ya Nkomo tarafa ya Kilenchune – Tigania Mashariki alisomea katika shule za Lubunu Primary, na St Kizito Secondary (O Level) na Friends School, Kamusinga (A Level).

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi mnamo 1987 alikohitimu Shahada ya Ualimu akimakinikia masomo ya Kiswahili na Jiografia. Mnamo 1995, alijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton alikosomea shahada ya uzamili na Uzamifu.

Prof Mukuthuria aliwalea wataalamu wengi chipukizi waliopitia katika mikono yake. Alikuwa na kalamu yenye utelezi mno na hivyo basi kuchangia zaidi ya makala 30 ya kitaaluma yaliyochapishwa katika majarida mbalimbali ulimwenguni – barani Afrika, Asia, Ulaya na Marekani.

Kaulimbiu aliyoichangamkia mno katika uhai wake ni kwamba maarifa na habari ni mambo ambayo hayakuwa na umuhimu wowote yakihodhiwa na mtu mmoja.

Aliamini kwamba vitu hivyo vilikuwa muhimu kwa jamii pindi vingesambazwa na watu wengi kuvipokea. Kwa hiyo, Prof Mukuthuria alikuwa radhi kuwagawia wataalamu wengine kanzi ya taarifa kutoka kwenye maktaba yake kubwa.

Taaluma ya Kiswahili imempoteza msomi wa isimu ambaye alitegemewa sana. Marehemu atazikwa tarehe 4 Jumamosi ijayo, 2018, Jumamosi ijayo.

Buriani ‘mufti’.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katicha Chuo Kikuu cha Chuka

[email protected]