Makala

KAULI YA MATUNDURA: Yakini, mikondo ya makuzi ya kamusi za Kiswahili Afrika Mashariki inatia moyo

October 9th, 2019 2 min read

Na BITUGI MATUNDURA

WAKATI wowote kuanzia sasa, toleo la 3 la Kamusi ya Karne ya 21 (Longhorn Publishers ) litatoka kwenye matbaa.

Nilikuwa mmoja wa wahariri waliotwikwa jukumu la kushiriki katika mchakato wa kuandaa toleo la kwanza la kamusi hiyo iliyotolewa kwa mara ya kwanza mnamo 2010.

Aidha hivi majuzi nilipata fursa nyingine ya kuipitia kamusi hiyo na kushuhudia jinsi ilivyokua na itaendelea kukua kadri miaka inavyosonga.

Kwenye ripoti yangu kuhusu kamusi hii, nilitanguliza shukrani zangu kwa kampuni ya Longhorn Publishers PLC kwa kunipa fursa ya kuipitia Kamusi ya Karne ya 21 (Toleo la 3).

Kuna historia ndefu baina yangu na mradi wa kuiandaa kamusi hii tangu 2009 jinsi ambavyo nimekwisha kutaja.

Meneja wa Vitabu vya Sekondari, Bw James Mwilaria alinitwika majukumu manne mazito kuhusiana na kazi hii ya Toleo la 3; nayo ni: Kuhariri na kuiboresha Kamusi ya Karne ya 21 (Toleo la 3), kupunguza idadi ya kurasa kwa baina ya kurasa 80 – 100, kuongeza vidahizo vyovyote vipya ambavyo vinaweza kuwa havikuingizwa katika Toleo la 3, Kutoa maoni yoyote ya matini za nyongeza ambazo zinaambatana na sheria za leksikografia. Nilifahamishwa kwamba madhumuni makuu yalikuwa ni kupunguza kurasa na ‘kubana matini’ ili iwe faafu zaidi. Aidha nilitwikwa jukumu la kutoa mapendekezo mengine muhimu ya kuiboresha kamusi.

Kwa hiyo, ripoti hii inaangazia majukumu niliyofanikiwa kuyatekeleza na vipi na yale ambayo sikufanikiwa kuyatekeleza na kwa nini.

Katika kutekeleza jukumu la kwanza, ilinilazimu nipitie kila kidahizo na namna kilivyotomeshwa (kilivyotolewa maelezo ya kiufafanuzi kwenye kamusi).

Niliongeza ufafanuzi pale ambapo nilipohisi kwamba dhana fulani au neno fulani la kimsingi linalochangia kueleweka kwa kidahizo limeachwa nje. Kadhalika, nilifanya marekebisho ya tahajia au vinginevyo pale ambapo ninahisi kwamba haikuwa sawa.

Katika kutekeleza jukumu la pili la kupunguza idadi ya kurasa kwa baina ya kurasa 80 – 100 nilihisi kwamba Kamusi ya Karne ya 21 tangu awali ilikuwa na mambo yaliyoifanya kuwa na upekee ikilinganishwa na kamusi nyingine zilizoitangulia au zilizoifuatia.

Kamusi ya Karne ya 21 ina nyongeza ya taarifa ambazo kimsingi zinapaswa kuwa katika kamusi za taaluma au nyanja fulani mahususi. Kadri taarifa hizi zilivyozidi kuongezwa ili kuipa kamusi hii upekee wa namna fulani, ndivyo kurasa zake zilivyozidi kuongezeka.

Kwa hiyo, nilipendekeza kwamba kuipunguza kamusi hii kwa kurasa takriban 80 – 100 ina maana kuwa taarifa hizo ziondolewe.

Kurasa hizi haziwezi kupunguzwa kwa kuondoa baadhi ya vidahizo au maelezo ya vidahizo hivyo. Kufanya hivyo kutaifanya Kamusi ya Karne ya 21 (Toleo la 3) kuwa dhaifu zaidi.

Isitoshe, makuzi na uimarikaji wa kamusi huonekana kupitia kwa kuongeza maneno mapya au yale yaliyosahaulika kila inapotolewa upya – wala si kuondoa taarifa muhimu.

Aidha, nyongeza ya taarifa fulani inatokana na misukumo ya soko ambapo watumiaji wa kamusi hutaka taarifa fulani ziingizwe kwenye toleo jipya la kamusi kama hii. Kwa hiyo, ikiwa lengo hili ni lazima litekelezwe kwenye Kamusi ya Karne ya 21 (Toleo la 3).

Aidha niliingiza na kutomesha maneno machache ya kimsingi ambayo nilihisi ni muhimu.

Vinginevyo, nilihitimisha kwamba kazi nzuri sana ilifanywa katika kuyaingiza na kuyafafanua maneno ya Kiswahili katika Kamusi ya Karne ya 21 (Toleo la 3). Ninasubiri kwa hamu na ghamu kuchapishwa kwa toleo hilo la tatu la kamusi hiyo.

 

[email protected]