Makala

Kauli ya wakulima wa maparachichi Kenya kuhusu soko la China

May 25th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

APRILI 2019, serikali ya Kenya ilitia saini mkataba baina yake na China, utakaowezesha wakulima wa humu nchini kuuza maparachichi katika taifa hilo.

Mkataba huo, umeifanya Kenya kuwa nchi ya kwanza Afrika kuuza maparachichi Barani Asia, lenye walaji zaidi ya bilioni 1.4 wa matunda haya.

Uliafikiwa na Rais Kenyatta na mwenzake wa China, Xi Jinping, alipofanya ziara nchini humo ya kuimarisha uhusiano mwema wa kibiashara na Kenya.

Wakulima wa maparachichi humu nchini, wanatarajiwa kuuza zaidi ya asilimia 40 ya matunda haya China.

“Makubaliano haya yamejiri kufuatia mikakati mirefu ya kuyaidhinisha, na wataalamu wa kilimo China kuzuru wakulima wa maparachichi Kenya. Yakitekelezwa kikamilifu, soko la China litanunua zaidi ya asilimia 40 ya matunda haya yanayozalishwa Kenya,” ilieleza taarifa ya Ikulu ya Rais iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Katika siku za hivi karibuni, serikali imekuwa ikihimiza wakulima kukuza maparachichi kwa wingi.

Kuna aina tofauti ya maparachihi kama vile Hass, Fuerte na X-ikulu, kundi hili likiwa ni yale ya kisasa – chotara.

Ni mkusanyiko wa maparachichi yaliyojaamishwa kupata moja maalumu.

Pia, kuna yale asili, yaliyooanza kupandwa kitambo.

Humu nchini, yanayopandwa kwa wingi ni Hass.

Aidha, wakulima wengi wameacha kukuza mimea mingine ili kuzamia kilimo cha Hass, kwa sababu ya faida zake kimapato ndani na nje ya nchi.

Mkataba wa Kenya na China kuimarisha soko la matunda haya ukionekana kuleta nafuu kwa wakulima, serikali ingali na kibarua ili kuafikia kiwango cha zaidi ya asilimia 40 ya mazao inachotaja yatauzwa nchini humo.

Kwenye mahojiano na baadhi ya wakulima wa maparachichi, wanalalamikia kupanda kwa gharama ya kufanya kilimo nchini hasa pembejeo.

“Upanzi wa matunda haya, hatua za kwanza hutumia mbolea hai (ya mifugo na kuku). Ili kuongeza mazao, miparachichi inahitaji kuwekwa fatalaiza ya kisasa na ambayo ni ghali mno,” anasema Bw Apollo Maina, mkulima wa maparachichi ya Hass, Kigumo kaunti ya Murang’a.

Fatailaza bora-yenye madini kamilifu, mfuko wa kilo 50 unagharimu zaidi ya Sh3, 000 na kulingana na Bw Maina gharama hii imezima ndoto ya wakulima wengi kufanya zaraa.

“Serikali inapaswa kutathmini gharama ya kufanya kilimo, haswa kwa kushusha bei ya pembejeo ambayo ni ghali mno,” anahimiza mkulima huyu.

Miparachichi ikiwa imezaa maparachichi. Picha/ Sammy Waweru

Pembejeo inajumuisha mbolea, mbegu na dawa.

Ni muhimu serikali kutoa mbegu za matunda haya zilizoafikia ubora wa bidhaa za kilimo, kulingana na Boniface Ngacha ambaye pia ni mkulima wa maparachichi Kirinyaga.

Mkulima huyu anasema wengi wameshindwa kufanya ukuzaji wa maparachichi kwa sababu ya kuwepo mbegu za hadhi duni.

“Sokoni kuna mbegu nyingi sana duni na ni wajibu wa serikali kutufadhili mbegu zilizoafikia ubora wa bidhaa,” anaeleza Bw Ngacha.

Shirika la kitaifa la utafiti wa kilimo na ufugaji nchini (Karlo) na la ubora wa mimea (Kephis), ndizo taasisi zilizotwikwa jukumu na serikali kuangazia masuala ya kilimo nchini, hivyo basi ndizo zinapaswa kutoa mwelekeo wa mbegu bora.

Taasi hizo zinapaswa kushirikiana na ile ya kutathmini ubora wa bidhaa (Kebs).

“Kinacholemaza juhudi za wakulima wengi ni kukosa kubaini mbegu na mbolea bora. Kabla ya kuingilia kilimo, ni muhimu kuangazia vigezo hivyo,” anashauri Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya kilimo hasa matunda.

Ili kufanikisha soko la maparachichi Uchina, mdau huyu anahimiza serikali kuwa na mpangilio maalum wa kukusanya mazao.

“Kwa ushirikiano na serikali za kaunti, ibuni mashirika yatakayokuwa yakikusanya mazao ili kuepuka kero la mawakala,” anapendekeza Bw Mwenda.

Wakulima pia wanashauriwa kujiunga na vyama vya ushirika, ambavyo husaidia kutafuta utafutaji wa soko la mazao.

Miundo msingi kama vile barabara bora ni suala lingine ambalo serikali inafaa kutilia mkazo.

“Baadhi ya barabara mashinani hazipitiki, hasaa msimu wa mvua. Mashambani ndiko kilimo kinafanyika. Tukivuna inakuwa vigumu kusafirisha mazao,” Bi Agnes Karira, ambaye ni mkulima wa matunda eneobunge la Mathira Nyeri, maparachichi yakiwemo, akaambia Taifa Leo.

Juhudi zote hizo zitakuwa bure bilashi endapo mkulima hatakuwa na kiini cha maji. Mpango wa serikali kuchimba mabwawa ya maji katika kila kona ya nchi, itapiga jeki uzalishaji wa matunda haya kwani wakulima wataweza kutumia mfumo wa kunyunyizia mashamba maji kwa mifereji.

Maeneo yanayozalisha maparachichi kwa wingi nchini ni; Muranga, Kisii, Nyeri, Kirinyaga, na Embu. Kericho, Kiambu, Meru, maeneo ya Ukambani na sehemu kadhaa Bonde la Ufa, pia hukuza matunda matunda haya.