Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Benki: Kelele za mlango katu haziniasi usingizi

July 3rd, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

KWA sababu siku hizi nimekuwa sugu wa uchambuaji na uchambaji wa mahasidi, sikukosa usingizi niliposhutumiwa na baadhi ya watu waliodai Benki Kuu ya Kenya ilikosea kuandika neno “Banki” kwenye sarafu mpya.

Kelele za mlango haziniasi usingizi.

Mtu mmoja aliyejiambika jina la kupanga ili asijulikane alitangaza kwa umma mpana kupitia jukwaa la twitter kwamba nimelipwa na serikali kuitetea katika matumizi yake ya neno Banki badala ya Benki.

Ilmradi mimi nimekuwa msemaji wa serikali, msemaji ambaye kazi yake kubwa ni kusema uongo, kusema zuri ni baya na baya ni zuri? Na serikali imenilipa fedha kiasi gani? Ujuzi wangu dhalili wa Kiswahili nimeuza ghali au kwa bei tahafifu?

Kadiri ninavyosikiza maoni ya wachambuzi na wachambaji, ndivyo ninavyoona msingi wa msimamo wao: wanasema kwamba benki ni sahihi, sio kwa sababu ni sahihi tu, bali zaidi kwa sababu wanalitumia Watanzania.

Mbona Watanzania wengi wanasema bidhaa “feki” kwa maana ya “counterfeit” badala ya “bandia” au “ghushi.” Kwa hiyo tuharamishe matumizi ya maneno mbadala haya, “bandia” na “ghushi?”

Baadhi ya Watanzania hupenda kusema “menejimenti” kama tafsiri ya neno la Kiingereza “management” badala ya “usimamizi” au “utawala.” Je tupige marufuku matumizi ya “usimamizi” au “utawala” kwa sababu hawayatumii Watanzania fulani? Zingatia kwamba ninasema Watanzania fulani au baadhi ya Watanzania.

Hii ina maana kwamba si kila Mtanzania anatumia maneno feki na menejimenti.

Kwa wanaoyapenda maneno haya, wala hayana ukakasi wa aina yoyote. Yanawatirikia kwenye ndimi kama asali iliyorinwa jana.

Kwa watu wengine, kushurutisha maneno haya yenye asili ya Kiingereza kuwa sehemu ya msamiati wa Kiswahili ni kero kubwa.

Isitoshe, Tanzania inavyo “viswahili” mbalimbali na hili kiisimu ni jambo la kawaida kabisa.

Mathalani ni Wanzabari ndio waliosisitiza kwamba East African Kiswahili Commission iitwe Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA).

Labda nitaje kwamba ufupisho KAKAMA tumeuundia Arusha mnamo 2016 tukiwa tunapitia mpango mkakati wa Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.

Mdogo kama sisimizi

Wahusika walikuwa ni Prof Kimani Njogu, Dkt Anne Mishe, Victor Elia, Dkt Simon Sewangi, Katibu Mtendaji wa KAKAMA Prof Kenneth Inyani Simala na mimi hapa mwenzenu mdogo kama sisimizi.

Lakini hivi karibuni nilipokuwa ziarani Dar es Salaam mwandishi wa gazeti la Mwananchi Solomon Gadi aliniuliza kuhusu wapi lilipotokea neno Kamisheni.

Yaani kwake kama Mtanzania wa Tanzania bara Kamisheni haliingii akilini, neno mwafaka ni Tume.

Kwa kweli “tume” ndivyo ambavyo Wakenya hutafsiri neno “commission.” Kwa hiyo, neno “tume” liwe kosa kwa sababu Wazanzibari hawalitaki, lina ukakasi kwao? Au je, Kamisheni liwe kosa kwa sababu Wakenya na Watanzania bara wanalipenda “tume”?

Rafiki yangu Omar Babu au Abu Marjan aliyetuacha mkono alikuwa akiniambia tena na tena “jibu la mjinga sukuti.”

Leo nimeamua kwenda kinyume na ushauri wake, lolote na liwe.