Makala

KAULI YA WALIBORA: Dhana kwamba ufahamu wa lugha aghalabu ni kigezo cha maarifa katika fani yoyote ile inapotosha

March 16th, 2018 2 min read

Na PROF KEN WALIBORA

Nilitumia treni ya SGR kwa mara ya kwanza wiki iliyopita. Safari yangu ya kwenda Mombasa kutoka Nairobi na kurejea tena Nairobi ilikuwa raha ilioje! Raha ya kulimbuka kufanya jambo usilowahi kulifanya tena.

Nimewahi kusafiri kwa treni ya mwendo wa kobe ya zamani zile za ujana wangu. Ila mara hii nilifaidi mno mandhari nzuri ya nyika na mifugo na wanyama pori. Isitoshe, behewani abiria wakipiga soga kwa raha zao.

Nimewahi kusafiri kwa treni Ulaya na Marekani. Sijaona watu wasiojuana hata ahlan wasahalan wakipiga soga safarini. Ni kila mtu na hamsini zake. Unapowaona watu wanazungumza sana na ndiyo mara ya kwanza kukutana ndipo unapotambua kwamba Afrika ni tofauti na mabara mengine. Kimsingi Mwafrika kwa kadiri fulani bado anadumisha “ujamaa” ambao ni sifa bainifu ya utu wake, ubinadamu wake.

Safarini nilisema na watu wengine nisiowajua. Tulisema kuhusu mada mbalimbali; si hatima ya mwanadamu duniani, si usasa, si falsafa, si uchumi, si uhusiano wa mataifa, si ukabila si elimu.

Ili kugeuza safari yangu darasa zuri la elimu, nikisikiliza zaidi kuliko kusema. Miongoni mwa “walimu wangu” alikuwapo mwanaume mmoja wa makamo. Hatukuambiana majina ila alisema nami sana tulipokuwa kwenye mkahawa wa treni.

Alianza mazungumzo kwa Kiswahili kizuri sana. Punde si punde akachupia Kiingereza alichokisarifu si haba. Akabaki papo papo pa Kiingereza, habanduki katu.

Katika yote lililonishtua kama kauli yake kuhusu nchi ya Tanzania.

Alisema alikwenda Tanzania akakutana na watu wasioweza kuzungumza Kiingereza. Alishangaa mwalimu wangu huyo wa treni; “Nchi itaendeleaje bila wenyeji kusema Kiingereza?” Kwake yeye ni kosa kubwa kwa Watanzania kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia masomo mbalimbali tokea chekechea hadi chuo kikuu.

Wanahitaji kutumia Kiingereza ili wapige hatua kubwa kimaendeleo. Hapo ndipo nilipomsahihisha kwamba kwa maoni yangu, kosa la Tanzania si kufundisha kwa Kiswahili.

Bali ni kuanza kwa kufundishia Kiswahili katika shule za msingi, kisha kuwalazimishia wanafunzi Kiingereza kama lugha ya kufundishia masomo mengine yote katika shule za sekondari.

Wanafunzi waliozoea kujifunza kwa Kiswahili katika shule ya msingi, hutatanika na kutatizika wanapokumbana na Kiingereza ghafula bin vuu.

Nilimwambia kwamba kwa maoni yangu Tanzania inapaswa kuamua kama inataka ama Kiswahili au Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia katika mfumo wa elimu tokeo mwanzo mpaka mwisho. Kuna hekima katika msemo usemao, “Mzoea kupanda punda, farasi hamwezi.”

“Mwalimu” wangu alishangaa kwa kauli yangu. Hakukasirika ila alimaka na kuendelea kunidadisi zaidi. Nami nikaamua kumdondolea mwalimu ziada ya maoni yangu ya kinyonge.

Nikamwambia kujua Kiingereza sio kigezo cha maarifa. Wakorea, Wachina na Wajerumani hujifunza sayansi na masomo mengine kwa lugha zao. Maarifa hayafungamanishwi na Kiingereza tu. Sayansi ni maarifa si lugha na kwa hiyo hata Kiswahili kinaweza kubeba uzito wa sayansi, na hisabati na teknolojia.