Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Fahari iliyoje Fasihi ya Kiswahili nayo pia kutafsiriwa!

February 27th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

BAADHI ya vitabu bora nilivyowahi kuvisoma havikuandikwa kwanza katika lugha ninayoelewa.

Mathalani nilikumbana na riwaya za mwandishi Mrusi Leo Tolstoy kama vile War and Peace na Anna Karenina nikakorwa na ubora wa kisanii.

Lakini Tolstoy aliziandika riwaya zake katika Kirusi nisichokijua. Hizi riwaya za raghba kubwa zinazosheheni maudhui mbalimbali yakiwemo mahaba na vita, zimenifikia mimi na wengine wengi kwa sababu ya mzungu wa tafsiri.

Nasisitiza kwamba tafsiri ni mzungu, tena mkubwa sana kwa maana unaweza mawasiliano kati ya lugha mbili mfaraka, kila lugha ikifumbatwa na kanuni miundo na tamaduni zinazokinzana na nyingine.

Profesa Ken Walibora. Picha/ Maktaba

Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere naye alifanikiwa kutuletea ukwasi wa ubunifu wa William Shakespeare kwa kuzitafsiri kazi zake mbili kwa Kiswahili, yaani Juliasi Kaizari na Mabepari wa Venisi.

Nakumbuka furaha yangu kuzisoma kazi hizi za Shakespeare katika Kiingereza, ‘Julius Caesar’ na ‘The Merchant of Venice’ na kuzilinganisha na tafsiri ya Mwalimu Nyerere.

Kama anavyodai Prof Alamin Mazrui, tafsiri za kazi za fasihi kutoka kwengineko zilipata kujumuishwa katika fasihi ya Kiswahili.

Hata katika mfumo wa elimu, wakati vitabu vya kutahiniwa vilivyoteuliwa kwa ajili ya somo la fasihi ya Kiswahili, zilikuwamo tafsiri za Kiswahili kama vile Mfalme Edipode, tafsiri ya Samuel Mushi ya tamthilia ya Myuyani Sofokile iitwayo ‘Oedipus Rex’ au ‘Oedipus the King’. Hata tafsiri za Nyerere za kazi za Shakespeare ziliingia katika tapo la fasihi ya Kiswahili.

Kutafsiriwa kwa kazi za kwengineko kwa Kiswahili ni jambo zuri.

Mwanzoni hilo tu ndilo lililokuwa likifanyika. Hata maandiko matakatifu kama vile Biblia na Kurani yalitafsiriwa kutoka kwa lugha hizi hadi kwa Kiswahili kwa ajili ya hadhira za Kiswahili.

Hata hivyo, haki inasema haifai tafsiri kwenda upande mmoja; kutoa ni kikoa, ukipokea nawe toa.

Kwa hiyo juhudi za kutafsiri kazi za Kiswahili kwa lugha nyingine za dunia zimekuwa zikifanywa, nazo zinastahili kupongezwa.

Ebrahim Hussein, bilmathalani, alitafsiri tamthilia yake ya Kinjeketile kwa Kiingereza naye Kimani Njogu akimtafsiria Mashetani kwa Kiingereza pia.

Baadhi ya kazi za Shaaban bin Robert zimetafsiriwa kwa Kijerumani, Kifaransa na Kitaliano. Vile vipo kazi za Said A. Mohmed ambazo nazo zimetafsiriwa katika lugha kadha za Ulaya.  Mathalan tamthilia yake ya Amezidi umetafsiriwa kwa Kiingereza na kuwa He is too Much.

Nilikuwa siku zote nikitaraji kazi yangu moja muhimu itafsiriwe, wasomaji wa lugha nyingine wafaidi uhondo.

Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) lilitafsiri hadithi yangu ya Kiingereza ‘Bobby the Dog’ hadi kwa Kiswahili nikafurahi sana.

Nami mwenyewe katika unyonge wangu nilijikusuru kutafsiri hadithi ya watoto ya ‘Ndoto ya Amerika‘ hadi kwa Kiingereza.

Na sasa nimefurahi kupata nakala zangu za awali za tafsiri ya riwaya yangu ‘Siku Njema’ kwa Kiingereza.

Kiswahili kinaendelea kutoa, si kupokea tu.

“Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara