Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Fasili ya neno 'binamu' inavyoibua mtanziko

February 6th, 2019 2 min read

NA PROF KEN WALIBORA

Nini maana ya neno “binamu” katika Kiswahili? Je, ni kisawe kabisa cha neno la Kiingereza “cousin”? Watafsiri wa Neno: Biblia Takatifu wanafasili “binamu” katika sherehe ya tafsiri yao kuwa “mtoto mwanaume wa ndugu mwanaume wa baba.”

Kwao wao nasaba ya kuumeni na jinsia ya mhusika ni vigezo muhimu katika kubainisha nani hasa binamu. Ina maana kwamba kwa mantiki hii mtoto wa kike wa amu hawezi kuwa binamu wala mtoto wa shangazi au mtoto wa mjomba, si hoja nini jinsia yao.

Kwa fasili hii, Watafsiri wa Neno:Biblia Takatifu wanawiana kidogo na fasili ya Kamusi Elezi. Wao nao wanasema binamu ni:” mtoto wa ndugu wa kiume baba. Hata hivyo, kwao jinsia ya mtoto mwenyewe si muhimu, muhimu ni kwamba ni mtoto wa nasaba ya kuumeni ila si mtoto wa shangazi.

Kamusi ya Karne ya 21 nayo inasema binamu ni “mtoto wa shangazi au mjomba.” Kwa hili inafanana na Kamusi Kuu inayosema binamu ni “mtoto wa kike au wa kiume wa shangazi au mjomba.

“Kamusi hizi mbili, yaani Kamusi ya Karne ya 21 na Kamusi Kuu hazizingatii jinsia ya mtoto mwenyewe wala haizingatii kama ni mtoto anayetokea kuumeni au kukeni katika nasaba.

Hata hivyo zinamwondoa mtoto wa amu katika kijelezi hiki cha “binamu” na hivyo kupingana na fasili ya Kamusi Elezi na watafsiri wa Neno: Biblia Takatifu.

Aidha inakwenda kinyume kabisa na Kamusi ya Kiswahili Sanifu (toleo la pili), inayosema binamu ni “mtoto wa ami” au Kamusi ya Kiswahili Fasaha inayosema binamu ni “mtoto kiume wa baba mkubwa au mdogo.” Na kwa hapa watungaji wa Kamusi ya Kiswahili Fasaha wanazingatia jinsia ya mtoto na mzazi.

Kufikia hapo umeona mkanganyiko uliopo? Je, umechanganyikiwa kama mimi? Kusema la kweli sielewi kabisa wala sijui nimwamini nani katika hawa wote wanaojaribu kutufafanuliwa maneno ya Kiswahili.

Nilianza kwa kuuliza je, binamu ni kisawe cha neno la Kiingereza “cousin?” Inawezakana kwamba kwa baadhi yetu vivuli vya maana tulivyo navyo vimeathiriwa na uelewa wetu wa maana ya hili neno la Kiingereza.

Wasemaje wa Kiingereza huwa hawana shaka wanamaanisha nini wanapolitumia neno lao. Ila sisi wasemaje wa Kiswahili tunawayawaya tu kama fasili hizi zinazokinzana zinavyothibitisha.

Hata baadhi ya wasemaji wa Kiswahili wanapozungumzia “shangazi” na “mjomba” huwa wanafikiria ni visawe vya maneno ya Kiingereza “aunt” na “uncle.” Mawe!

Nimewahi kulijadili suala hili katika safu hii ila kwa sasa naligusia tu kutanua mawanda ya mdahalo huu wa utata wa matumizi katika lugha ya Kiswahili.

Hapana shaka haya ni baadhi ya mambo yanayowatanza watumiaji wa Kiswahili. Ni sawa kama wasemaji limbukeni wanakosea. Lakini inakuwaje pindi kamusi zinapokinzana na kuwapotosha watumiaji?

Haiwezekani kuwa na midahalo na maafikiano mwafaka kuhusu baadhi ya maneno haya? Jamani tuondeleeni kero.