Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Heshima ya watoto wa Arusha ni ithibati kuwa dunia hii si tenge tahanani kila mahali

April 17th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

NIMEKUWA katika mji wa Arusha kwa zaidi ya wiki nzima.

Ni shughuli za Kiswahili ndizo zilizonipeleka.

Nitayakumbuka mengi niliyoyaona huku ila “shikamoo!” za watoto wa Arusha zitaselelea daima katika kumbukizi zangu. Ukiwa mtu mzima kila ukikutana na watoto wanakusalimu “Shikamoo!” “Shikamoo!” kwa heshima zote.

Kama ulifikiria huna thamani tena maisha nenda Arusha watoto wa huko wakusalimu “shikamoo!” Utapata kujiamini tena na kujithamini tena.

Hitimisho langu ni kwamba watoto wa Arusha wamethibitisha tena kwamba bado kuna utu na adabu duniani, kwamba dunia hii si mchafuge kila pahali, si tenge tahanani kila mahali.

Kuna maeneo mengine ya dunia watu bado wana ubinadamu wao.

Hivi watoto wa Arusha walipata wapi utashi na uzoefu wa kuwaambia wakubwa zao, hata watu ajinabi kama mimi,

“Shikamoo!” Maamkuzi yao ya taadhima yamepatikana kwa sadifa au nasibu tu? La! Hasha!

Wamezaliwa wakalelewa na kukulia katika mazingira yenye heshima kwa watu wazima.

Wamenikumbusha enzi zangu utotoni pale watoto walipolazimika kusimama kwenye basi au matatu pindi mtu mzima au mjamzito alipokosa pahali pa kukaa garini.

Heshima iliwasukuma kusimama kwa hiari bila kushikiwa shokoa. Labda ndipo wahenga wa Kiswahili wakasema: “Mtoto uleavyo ndivyo akuavyo” au “mwana hutizama kisogo cha nina.”

“Shikamoo” za watoto wa Arusha na marahaba za watu wazima zimenifanya kuonea raha heshima na kufaidi uhondo na utamu wa Kiswahili kizuri.

Heshima na uhondo wa Kiswahili vimekutana na kuunda mseto wa mazingira mwafaka ya mtu kuishi, mtoto na mtu mzima. Hiki Kiswahili kina raha ati, hasa kinapopata msemaji mahiri na watu wa Arusha—watoto na watu wazima hawakupungukiwa kwalo.

Kiswahili kingekuwa kinasemwa hivyo Machakos au Mandera mbona ningefurahi si haba.

Kwa nini watoto wa Afrika Mashariki wote wasifundishwe kama watoto wa Arusha kuwasilimu wazee, wenyeji na wageni pia, “Shikamoo?” Katika umri wa makamo niliofika, kuna unyeti sana katika kuitwa mzee.

Watu hawataki kuzeeshwa mno maana hilo linawakumbusha kifo kinavyojongeajongea karibu. Bado mimi hushtuka kidogo nikiitwa mzee.

Lakini kama kwa kunisalimu marahaba watoto wa Arusha wamenizeesha, basi acha nizeeshwe nizeeke.

Basi kuna upande mwingine wa sarafu. Rafiki yangu mmoja naye alinisimulia mtagusano wake na mtoto mmoja wa Arusha miaka kadha iliyopita.

Bendera za mataifa yote sita ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zilisambazwa miongoni watoto mjini Arusha.

Mtoto mmoja mdogo aliyepewa bendera ya Kenya alimwendea rafiki yangu na kusema anataka abadilishiwe awe na bendera ya Tanzania. Rafiki yangu alipomdadisi yule mtoto mdogo alitamka waziwazi: “Siwapendi Wakenya; nasikia ni mafisi hawa.”

Sasa huyu mtoto mwema kapata wapi habari kwamba Wakenya ni mafisi? Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo na mwana hutazama kishogo cha nina.

Watoto hukua wakichukia wale watu ambao wazee wao wanawachukia. Malezi ya shikamoo yanakula sahani moja na malezi ya hasama na husuda!