Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Huenda sera duni ya elimu Tanzania inaua watoto kilugha

May 29th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

PROF F.E.M.K. Senkoro alinishtua sana alipoandika makala kuhusu mauaji ya halaiki ya watoto wa Tanzania katika makala moja nilikumbana nayo mtandaoni zaidi ya miaka minane iliyopita.

Kwa kukiona tu kichwa cha makala yake, “Udadisi: Mauaji ya Halaiki ya Watoto wa Tanzania”, nilijiuliza nani huyo katekeleza mauaji haya ya halaiki ya watoto wa Tanzania, na kwa nini?

Nilipomaliza kuyasoma nikaelewa kwamba mtaalamu huyu mahiri wa fasihi hakuwa amebabaisha wala kutia chuku mno katika kauli yake.

Alikuwa analalamikia mfumo wa elimu Tanzania na suala la lugha ya kufundishia.

Prof Senkoro alikuwa akitoa maoni kuhusu tafiti zinazohusu lugha ya kufundishia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale ambapo wanafunzi wanafundishwa kwa Kiswahili katika shule za msingi na kulazimishwa kufundishwa kwa Kiingereza pindi wanapoingia shule za upili.

Hilo suala nimeligusia kidogo katika makala yangu ya wiki iliyopita lakini naona nilirejelea kidogo kwa vile ufinyu wa nafasi kwenye safu haukuniruhusu kutaja vipengele muhimu vya mdahalo huu.

Ninachosema sasa ni kwamba Prof Senkoro anakuona huku kuwalazimishia watoto wa Tanzania kufundishiwa kwa Kiingereza kutoka sekondari kuendelea ni sawia na kuwafanyia mauaji ya halaiki.

Prof Senkoro ni mtaalamu wa fasihi kwa hiyo uteuzi wake wa sitiari ya mauaji, mauaji ya kimathali unaashiria hasira aliyo nayo kwa adhana na madhila ya watoto hawa.

Vizazi hata vizazi vya watoto wa Tanzania vinalemazwa na ukiukwaji huu mkubwa wa haki zao za kufundishwa katika lugha wanayoielewa.

Ndiposa Prof Senkoro anatoboa wazazi kwamba huenda serikali ya Tanzania imekuwa ikikiuka katiba yake yenyewe kwa kuwakosesha watoto hao Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika masomo yao katika mfumo mzima wa elimu.

Mimi mwenyewe nilifurahi serikali ya awamu ya tatu Tanzania ya Jakaya Kiketwe ilipotangaza kwamba hilo lingesahihishwa.

Niliandika makala zilizojaa matumaini na kuisifu Tanzania kwa hatua hiyo.

Maneno matupu

Sikujua kwamba matamko ya serikali ya Tanzania yalikuwa maneno matupu.

Watanzania walikuwa wanapakwa mafuta kwa mgongo wa chupa; serikali ilikuwa haina nia ya dhati ya kuwapa watoto wa Tanzania haki zao.

Hili lilinibainikia dhahiri nilipokuwa Tanzania hivi karibuni na kuwasikia wanafunzi wawili wa kike, waathiriwa wa mauaji ya halaiki ya kilugha, wakitoa hoja zao kwenye kongomano.

Watoto hao ‘waliouawa kimbari’ walisema kwa mihemko na fadhaa kwamba hawajielewi kabisa kwa mkanganyiko wa kilugha unaotokana na sera ya elimu Tanzania.

Mmoja wao alimwambia waziri wa elimu wa Zanzibar Mheshimiwa Riziki Pembe “elimu ya Tanzania ndiyo mbovu na mbaya zaidi duniani.”

Mimi nitakumbuka daima sio tu maneno ya wanafunzi hao bali namna walivyoyatoa kwa uchungu na hamaki maneno yale.

Wamechoka kuuawa kwa halaiki kilugha.

Sijui kama waziri Pembe anasikia anaelewa kilio cha wanafunzi hao.

Je, serikali ya Tanzania inasikia kilio cha watoto wanaouawa kilugha kwa sera duni ya lugha ya kufundishia?