Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Kazi za Fasihi husemezana na kuathiriana

April 24th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

NI vigumu kusoma tamthilia mpya ya ‘Usiniue’ ya Eric F. Ndumbaro na Maria N. Isaya bila kusikia mwangwi wa shairi la Abdilatif Abdalla la ‘Usiniuwe’ katika diwani yake maarufu ya ‘Sauti ya Dhiki’ aliyoitungia gerezani.

Si tu kwamba anwani ya tamthilia hii inalandana na anwani ya shairi la Abdilatif Abdalla bali pia kimaudhui kuna mshabaha mkubwa.

Tamthilia hii imesheheni mwangwi wa shairi, wala hilo tusilione la ajabu.

Kazi za fasihi husemezena na kuathiriana zenyewe kwa zenyewe kama mwananadharia Mikhael Bakhtin anavyodai kwa usahihi kabisa.

Kila tamko tusemalo ni tokeo la tamko la awali la mtu mwingine.

Hapa nitatoa mifano michache. Chinua Achebe alipoipa riwaya yake kichwa cha Things Fall Apart, alikuwa anabeba uteuzi wa maneno mateule ya mshairi Mwingereza William Butler Yeats.

Rocha Chimerah amefanikiwa sana kuandika majuzuu matatu ya riwaya ya Siri Sirini, kwa kuzingatia hadithi ya fasihi simulizi ya Fumo Liyongo.

Kwa hilo Chimerah kafuata nyayo za Bitugi Matundura na K.W. Wamitila ambao wametunga tanzu mbali mbali kutokana na hadithi ya Liyongo. Nami nilipotunga riwaya yangu ya awali ya Siku Njema nilikuwa nimechota kichwa cha shairi la Siku Njema kutoka kwa diwani ya Said A. Mohamed ya ‘Sikate Tamaa’.

Katika shairi lake la beti 29, Abdilatif kakipa sauti kiinitete ambacho bado hakijaumbuika kamili na bado hakijazaliwa ili kizungumze na mama mzazi, kumrai asikiue. Kitoto hicho chasema:

Kama hunitaki mama, piya waniuliyani?
Nakuomba nikisema, usiniuwe tumboni,
Mama nizae salama, kisha nitupe ndiyani,
Mja alo na huruma, an’okote kunileya.

Sauti ya kiinitete katika tamthilia ya Eric F. Ndumbaro na Maria N. Isaya inawiana na sauti ya kiinitete katika shairi la Abdilatif ingawa katika tamthilia tayari mama amezika utu na umama wake na kukiulia mbali kitoto ambacho bado hakijazaliwa.

Kwa maneno mengine, katika tamthilia tunakumbana na sauti ya kitoto kilichokwishauliwa kikatupwa kwenye lindi la choo ilhali katika shairi ukatili huu bado kutekelezwa.

Katika shairi kuna nia ya kuua ilhali katika tamthilia uuaji umekwisha tekelezwa.

Vyovyote viwavyo, nafsi neni katika tamthilia na shairi ni ithibati tosha ya ubunifu wa hali ya juu.

Mshabaha huu wa kimtindo unaoana na mshabaha wa kimaudhui.

Hapana shaka kufikia hapa ni dhahiri shahiri kwamba waandishi wa tamthilia hii wamelivalia njuga suala zima la utoaji mimba.

Lilikuwa suala nyeti katika enzi ya uandishi wa gerezani wa Abdilatif mwisho mwisho wa miaka ya 1960 na mwanzo mwanzo wa miaka ya 1970.

Takriban nusu karne baadaye bado suala hili la utoaji mimba ni suala nyeti.

Siku zote ni suala linalopambanisha haki za kuishi kwa kitoto kisichozaliwa bado na haki ya mwanamke kujiamulia hatima ya kilichomo ndani ya kiwiliwili chake.

Aidha, suala hili linawapambanisha waungaji mkono wa utoaji mimba na wapinzani.