Makala

KAULI YA WALIBORA: Kiswahili kingali halua katika uchanganuzi wa matangazo ya mpira

July 11th, 2018 2 min read

Na PROF KEN WALIBORA

Uchanganuzi wa soka kwa Kiswahili siku hizi ni jambo la kawaida katika runinga za Kenya. Zamani haikuwa hivyo. Nakumbuka wakati nilipoteuliwa kuchanganua mashindano ya soka la kombe la mataifa bingwa Afrika katika runinga ya KBC 1998.

Wenzangu walikuwa Uchi Unyebadi, Elias Makori na Amole Asiko. Siku hizo nilikuwa mtangazaji wa mpira redioni.

Wasemao husema “Kila mwacha samboye huenda ali mwanamaji.” Labda hilo ndilo liliwasadikisha wakubwa kwamba niliweza kuchanganua kandanda. Ila kwa sasa hivi sijui kama wasimamizi wa redio zilizoko wanaamini kwamba nina lolote liwezalo kuchangia katika soka.

Ila tuachie hilo mbali turejee kwenye suala la uchanganuzi wa soka kwa Kiswahili katika runinga. Siku hizo ilikuwa kama dhambi kuzungumza Kiswahili katika uchanganuzi au utangazaji runingani.

Kiswahili kilikuwa chatumika redioni, chombo cha walalahoi. Ndio maana nilikuwa natangaza mpira na Ali Salim Mmanga, Leonard Mambo Mbotela, Jack Oyoo Sylvester na marehemu Billy Omalla, hakuna aliyebisha.

Runinga ya KBC iliyokuwa ikirusha matangazo mbashara ya mpira ilikuwa imewaratibu watangazaji wawili wa Kiingereza, John Nyongesa na Bernard Otieno.

Basi katika uchanganuzi wa mechi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na wenyeji Burkina Faso niliamua mimi kusema Kiswahili. Nilifanya uamuzi huo mwenyewe na bila kumwarifu mwenyekiti wa jopo la wachanganuzi Amole Asiko.

Amole alishtuka kunisikia nasema Kiswahili. Alipigwa na kibuhuti kwa hilo maana alikuwa tayari amezoea kunisikia awali nikibambanya Kiingereza katika uchanganuzi wangu.

Ni raha ilioje kuona hatua kilizopiga Kiswahili kufikia sasa! Mathalan mnamo Jumatatu nimemwona Yoshua Makori wa NTV akiongoza jopo la wachanganuzi wa soka maarufu Jack Oyoo Sylvester, Hassan mwana wa Ali na Elias Makori.

Ni fahari kubwa jinsi gani kumwona Elias bado anachanganua michezo na safari hii kwa Kiswahili safi kama ambavyo amekuwa anafanya sikuzote kwa Kiingereza.

Ilikuwa raha kusikia maoni ya wachanganuzi yakiwatoka katika Kiswahili kinachoeleweka na kila mtu wakibashiri kuhusu nani zaidi kati ya Ufaransa na Ubelgiji au kati ya Croatia na England.

Isitoshe, ipo mizaha ambayo haiwezekani kutafsirika kwa Kiingereza na wachanganuzi wanafanya mawasiliano kuwa na uhalisi na uasilia zaidi wanapotumia lugha yao.

Inakuwa hivyo hata kwa wachanganuzi Waingereza wanapochambua soka katika lugha yao, mambo yanawatirikia kwa mazoea.

Linganisha uchanganuzi wa Jay Jay Okocha na Owen Hargreeves kwa mfano katika Super Sport. Huenda Okocha anaelewa soka zaidi kuliko Hargreeves lakini sharti Okocha ayatafute maneno ya kubeba mawazo yake. Hargreeves hana haja ya kuyatafuta maneno ya Kiingereza; ni kana kwamba tayari yapo kwenye ncha ya ulimi wake.

Wakati ninaandika makala hii hatujui bado matokeo ya washindi wa nusu-fainali ya kombe la dunia. Ila wakati wewe unaposoma labda tayari tuyajua.

Timu moja katika hizo itashinda kombe la dunia, na Kiswahili nacho kitashinda wachanganuzi wakiendelea kukitumia katika mawanda yote.