Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Lugha kwenye vyombo vya usafiri isitumiwe msobemsobe

May 8th, 2019 2 min read

NA PROF KEN WALIBORA

MTU anaweza kufanya utafiti kuhusu maandishi ya kwenye magari na kuibuka na ugunduzi mkubwa wa falsafa ya watu.

Kuna maandishi kwenye matatu, boda boda, bajaji, mabasi na malori. Mathalan, hivi majuzi nilipokuwa nimezuru Malindi niliona gari la matatu limeandikwa, “Wanaonichukia utawacost.” Nilipigwa na kibuhuti. Kwanza kwa sababu ya ujasiri wa nafsi neni katika kauli ile na pili nguvu za kuchanganya ndimi.

Je, ilikuwa kauli ya mwenye matatu hiyo inayohuduma kati ya Kilifi na Mariakani, au ni falsafa ya wahudumu tu?

Nini hasa kilichomfanya aiandike kauli hiyo kama alivyoaiandika? Je, kauli hiyo inatufundisha nini kuhusu hulka ya mwanadamu au tuseme jamii ya mwandishi wa kauli au aliyeamuru kauli hiyo iandikwe garini?

Huwezi kuisoma kauli hiyo bila kuona kwamba ni kitisho au tishio. Unausoma ujumbe na unakuchoma kama mshale wenye chembe cha sumu.

Msemaji hataki masihara; ukimchukia basi athari mbaya kwako. Kumbe chuki ina gharama ati! Kile ambacho kauli hiyo haisemi ni kwa nini achukiwe msemaji au nafsi neni? Kwani kafanya nini au kashindwa kufanya nini? Kupata nini au kakosa kupata nini?

Kwa nini wanadamu wanawachukia wenzao? Kwa nini watu wanachukiana? Kwa nini watu wengine wanachukiwa? Je, huyu anaweza kuwa kachukiwa kwa sababu ya mafanikio aliyo nayo na neema aliyoneemeshwa kwazo-neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo?

Na mbali na hayo kwa nini wakazi wa Afrika Mashariki wana mazoea ya kuandika ujumbe kwa mahasidi na mashabiki wao ili yasomwe hadharani na kila mtu?

Mambo yameanza kwa kanga na salamu zinazoandikwa kwenye kanga. Wanawake wa pwani hawanunui tu kanga msobemsobe; huwa wanatafiti kujua kanga zimeandikwa nini na hununua kuambatana na yaliyoandikwa. Mimi sijafanya utafiti wa kutosha ila nahisi kwamba baadhi ya salamu hizo huwa zimelenga mahasidi.

Ndio maana aghalabu utakutana na kauli kama: “Mchana mtasema na usiku mtalala.” Je, Kauli kama hiyo anaimbiwa rafiki? Je, kauli hii hasemi mtu anayesemwa semwa, aliyechosha na umbea wa wengine na kwa hiyo analisema la ili kuonesha hashtuliwi kama marehemu Esir alivyoimba “Hamtishi?

Lakini mtoa kauli wa barabara ya Kilifi kwenda Mariakani anachanganya Kiingereza ndani ya Kiswahili. Wanaonichukia utawacost. “Itawacost” ni ladha mpya ya Kiswahili jinsi kinavyoandikwa na hasa kinavyozungumzwa siku hizi.

Nimesema mara nyingi nami sichi kusema kwamba ipo siku utaitafuta sentensi ya Kiswahili iliyokamilika pasina neno la Kiingereza usiipate.

Itawacosti labda inayobebwa katika maandishi ya gari la matatu ya Kilifi kwenda Mariakani ni ithibati ya jinsi Kiswahili safi kinavyopotea, sikwambii ukali wa kitisho kilichodhamiriwa.

Katika hali halisi ya Uswahilini labda kauli hiyo ingekuwa: “Wanaonichukia watakiona cha mtema kuni” au kitu kama hicho.

Ila falsafa iliyoshika sasa ni kutohoa na kuchanganya msobemsobe. Ndiyo maana mpaka sasa sijui wanahabari wanamaanisha nini wanaposema “ handisheki.”