Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Msimamo wa Prof Ngugi kuhusu tija ya lugha asilia umebaki vilevile kwa muda tawili na umemrinia mengi

February 20th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

KINA CHA FIKIRA

HIVI karibuni katika mitandao kumezuka mdahalo mkali sana kuhusu utetezi wa Prof Ngugi wa Thiong’o wa lugha asili.

Ziara ya Prof Ngugi ya hivi karibuni ilihusisha kampeni kabambe ya kuzipigia upatu lugha za asili nyingine Kenya.

Hizi ndizo wengine wanaziita ‘vikabila’ kufuatia uundaji istilahi wa Kapinga.

Juma lililopita niliangazia mrejesho wa hadhira ya Prof Ngugi kuhusu taaluma ya tarjumi. Nilisema kwamba kwa nilivyoelewa mimi, baadhi ya wasikilizaji wake waliangazia namna alivyowasilisha kuliko kile alichokiwasilisha, huku wakimtarajia awe msemaji mwenye jazba kama PLO Lumumba au Barack Obama. Hii leo katika safu hii nataka nirejelea mdahalo wa lugha asili na uhusiano wake na Kiswahili na Kiingereza.

Prof Ngugi alizuru kwingi kuzindua vitabu vya shule za msingi vilivyoandikwa kwa lugha asilia.  Hata alihudhuria hafla ya uzinduzi wa vitabu vya rafiki yangu mwandishi  mmoja chipukizi huku Kisii mbali na kwingineko. Aidha alikutana na waziri wa elimu Amina Mohamed na kushauriana naye kuhusu tija ya ufundishaji wa lugha asili katika mtaala wa elimu.

Mwandishi Ngugi wa Thiong’o azindua ‘Kenda Muiyuru’ katika hoteli ya Sarova Stanley. Picha / Diana Ngila

Jambo moja ni dhahiri; msimamo wa Prof Ngugi kuhusu tija ya lugha asilia umebaki vilevile kwa miaka na mikaka, hauyumbiyumbi wala kutetereka. Sikuzote yeye amekuwa mstari wa mbele katika utetezi wa lugha asilia. Ndiyo maana alipopewa ufadhili wa kuanzisha jarida la kitaalamu katika katika Chuo Kikuu cha New York University (NYU) aliridhia kuanzisha jarida la Kigikuyu liitwalo Mutiiri.   Marehemu Prof Ali Mazrui alimkosoa sana kwa uamuzi wake. Badala ya kukipa Kiswahili kipaumbele, Ngugi alichagua lugha yake asilia.

Lakini kama wasemavyo wasemao, “Kipenda roho ni dawa” na kwake Ngugi dawa yake ni lugha yake asilia.

Tatizo la watu wengine ni kudhani kwamba Ngugi ndiye mtu wa kwanza kuzipa lugha asili za Kiafrika kipaumbele. Aidha Tatizo jingine ni kwamba si yakini kama Kiswahili kimo katika mkumbo wa  lugha asili za Kiafrika kwake Ngugi au wengine wanaopenda kuzivalia njuga lugha hizi. Je, Obi Wali hakuwa miongoni mwa watu wa awali kusema mnamo mapema miaka ya 1960 kuwa fasihi katika lugha za kigeni kama Kiingereza, Kifaransa na Kireno haina mashiko?  Wali alikuwa Mnaijeria aliyemzindua Ngugi na kumpa mbegu ya mwelekeo ambao amedumu nao tangu ujanani.

Hili la fasili ya lugha ya Kiafrika, lugha asili kwa maoni ya Ngugi lina utata kwake na kwa wengine. Lakini ikiwa tunamlaumu Ngugi kwa kukitelekeza Kiswahili tunapaswa kujiuliza: Kiswahili kimempa tija gani katika maisha yake ya usomi na uandishi? Je, Ngugi hajafaidi tija ya kutumia Kiingereza kama lugha yake ya ubunifu na hatimaye Kigikuyu? Kiingereza kimempa sifa na mirabaha mikubwa na haiba na kuchangia kusomwa na kutafsiriwa kwa vitabu vyake katika lugha mbalimbali duniani. Kigikuyu kimempa sifa na mirabaha kidogo. Kiswahili kimempa nini?

Mwamba ngoma huvuta kwake.

“Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara