Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Tulitafune hili fupa ‘etimolojia’

April 30th, 2019 2 min read

NA PROF KEN WALIBORA

MTU mmoja katika jukwaa la mtandaoni ameuliza majuzi neno la Kiswahili ‘marehemu’ lilitoka wapi? Unaweza kushangaa kwa nini mtu anajishughulisha na neno linaloambatana na kifo. Lakini ndivyo udadisi wa kiusomi ulivyo; watu huuliza maswali kuhusu chochote na lolote.

Sasa huyu anayevutiwa na marehemu amesukumwa na roho ya kiusomi kuuliza kuhusu usuli wa neno linaloelezea mtu aliyekata roho. Kwa maneno mengine, huyu mdadasi mwenzetu, anadadisi etimolojia ya neno marehemu.

Pindi tu alipotaja hilo akatokea mwingine aliyesema moja kwa moja kwamba swali hilo ni ithibati tosha kwamba kwa sasa lugha ya Kiswahili inahitaji Kamusi ya Etimolojia.

Sijui alichomaanisha mchangiaji huyu. Yaani anamaanisha kwamba tangu mwanzo hakuna Kamusi ya Kiswahili inayojaribu kueleza usuli wa maneno; etimolojia ya maneno?

Mbona ukitazama hata matoleo ya kwanza kabisa ya Kamusi ya Kiswahili Sanifu utakuta maelekezo ya baadhi ya usuli wa maneno! Hivi karibuni Kamusi Pevu ya Kiswahili ya K. W. Wamitila vilevile imeelezea usuli au etimolojia ya maneno mengi kabisa.

Mathalani kamusi hii inasema maneno kama vile dhahiri, dhahabu, dhabihu, dhakari, dhambi, dhalimu, dhamini na dhuluma, yametokana na Kiarabu (kwa ufupi Kar). Lakini vilevile kamusi hii inaonesha kuwa maneno kama diaspora, shati, skuli, na kabati yanatokana na Kiingereza (kwa ufupi Kng).

Kwa hiyo inashangaza kidogo kumwona mchangiaji anakimbilia kusema ipo haja ya kutungwa Kamusi ya etimolojia. Je, Kamusi zilizopo hazikidhi haja ya taaluma ya kietimolojia? Kama ndivyo ni sawa. Labda kwa kweli etimolojia ya Kiswahili inataka kufanyiwa udadisi na udadavuaji zaidi.

Kwa mfano, hitimisho la Wamitila kwamba diaspora ni neno linalotokana na Kiingereza unakubalika kwa kiasi fulani lakini Kiingereza nacho kimelikopa kutoka kwa Kigiriki ambacho kilitumiwa kuelezea kadhia ya msambao wa Wayahudi, au (Mayahudi) kutoka nchi yao asilia. Diaspora ni nomino ambayo inatokana na kitenzi diaspeirein lenye maana ya sambaa (kwa Kiingereza disperse).

Hili limenikumbusha jina la utani wanalolitumia wakazi wa Nairobi kuwaelezea wakazi wa Ongata Rongai; wanawaita watu kutoka diaspora sawia na Ongata Rongai wanakoishi.

Sawa na Wamitila anavyotomewa katika Kamusi yake, diaspora ni watu na pahali walipohamia. Ila katika muktadha wa Ongata Rongai, ni utani tu, si matumizi halisi.

Basi turudi kwenye etimolojia ya marehemu. Kamusi ya KKS ndiyo iliyotoa maelezo kwamba marehemu ni mhurumiwa, neno lenye usuli wa Kiarabu nasi tunaweza kukahitimisha kwamba linabeba mwonoulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu kuhusu hali ya mfu.

Yaani mfu anapaswa kuonewa huruma, kurehemiwa na Mwenyezi Mungu na kumghofiria madhambi yake duniani. Nimetumia “madhambi” makusudi kabisa hapa, ingawa najua askari sugu wa sarufi wasiojali Waswahili wenyewe husemaje, wapo tayari kunifanya marehemu kwa matumizi haya.

Mpaka sasa sijui kwa nini Ali Mtenzi alituletea mwendazake katika vyombo vya habari; neno ambalo linaendelea kuliua marehemu na kulizika katika kaburi la sahau.