Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Ustaarabu, kwa baadhi ya watu, ni kuisarifu lugha ya mkoloni kama wazawa, kisha kuutweza usuli wao

June 12th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

YAMKINI lugha za madola makubwa duniani zitaendelea kushamiri na kunawiri bila kizuizi.

Kiingereza chenye wasemaji asilia wachache kabisa kimekuwa ndicho Kiswahili cha dunia tangu Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Nyerere alipotoa kauli hiyo miongo mingi iliyopita.

Ubabe wa Uingereza ulichangia pakubwa kukieneza Kiingereza takriban katika kila pembe ya dunia.

Na kwa ukubwa wa dola simaanishi upana wa himaya bali satua na sauti katika maswala ya dunia.

Aidha sisemi kwamba Kiingereza kinasemwa na kuandikwa na namna moja. Hata kuhusu kile kinachofikiriwa kuwa Kiingereza sanifu, hapana mwafaka.

Wamarekani wana Kiingereza chao ambacho kwa matumizi, matamshi na hijai kinatofautiana na kile cha Waingereza.

Hata Waingereza na Wamarekani wao kwa wao wana Viingereza vingi tu vinavyotafautiana kulingana na mwahali na nyakati na tabaka au kitembo cha elimu.

Nchi zilizotawaliwa na Waingereza zote zinazungumza Kiingereza; si Naijeria, si Ghana, si Kenya si Uganda, si Australia.

Na kile nchi au kila sehemu katika nchi inakizungumza Kiingereza kwa namna mbalimbali, si sawa.

Unaweza mathalani ukabaini lafudhi ya Kiganda katika Kiingereza kulingana na namna msemaji anayetokea Uganda anavyoyatamka maneno ni vile anavyopandisha na kushusha kiimbo cha sauti yake.

Aidha akizungumza raia wa Naijeria, sisemi aliyezaliwa au kulelewa ughaibuni, aghalabu utabaini kwamba ni Mnaijeria huyo kwa lafudhi yake.

Sikijui Kifaransa ingawa nimewahi kusafiri hadi Ufaransa.

Ila naambiwa kwamba hicho nacho, kama Kiingereza na lugha zote nyinginezo, kina lafudhi na matumizi mbalimbali kutegemea alikotokea mtu.

Lakini Kifaransa hicho ni miongoni mwa lugha za madola makubwa, madola yenye uwezo, yaliyotawala maeneo kadha wa kadha katika enzi ya kikoloni.

Lugha nyingine za wakoloni ni pamoja na Kihispaniola, Kijerumani, na Kireno.

Zilizokuwa koloni za Uingereza, Uhispania, Ureno, Ufaransa na Ujerumani, mathalani zilishikiwa shokoa kuzungumza lugha za mabwana wakoloni hawa.

Kuona aibu

Ndiyo maana mpaka sasa kuna Wakenya wanaona aibu kuzungumza ama Kiswahili au lugha zao asilia; wanaona kwamba ustaarabu wao hauwaruhusu kusema lugha za kishenzi kama hizo.

Ustaarabu, kwao, ni kusarifu lugha ya mkoloni na kuitema kama mzawa. Wanajitenga kabisa na usuli wao.

Miaka mingi baada ya ukoloni mkongwe madola makubwa mengine yameanza kupenyapenya katika nchi maskini.

Kwa mfano, siku hizi tunanyweshwa Kichina kama dawa ya lazima bila kutarajia.

Wachina wakijenga barabara au reli wana tabia ya kuandika ilani na mabango kwa Kichina chao huku Afrika.

Ilani hizo na mabango hayo ya Kichina ni kwa ajili ya nani? Je, ni kwa ajili ya Wachina wanaofanya kazi ya kuuza mitumba sokoni Gikomba au nini?

Sina shaka kwamba ni muhali kwenda Uchina na kupata maandishi ya Kiswahili.

Kiswahili si lugha ya dola kubwa duniani. Wasemaji asili wa Kiswahili wanaweza kwenda China au Marekani wakajenga barabara au reli na kubandika huko mabango ya Kiswahili?