Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Yapo mafaa ya kuwapa majibu wanaosaka kujua

August 22nd, 2018 2 min read

NA PROF KEN WALIBORA

MNAMO Jumapili nilipokea swali kutoka kwa mtu nisiyemfahamu. Alikuwa anauliza swali: “Mtu aliyeajiriwa na magereza kutimiza hukumu ya kifo anaitwaje?”

Mwanzo sikujua kama nijibu au nisijibu. Mimi hukumbwa na mkururo wa maswali kutoka kwa watu ninaowafahamu na nisiowafahamu.

Baadhi yao hupenda tu kuniweka kwenye mizani waone uzito wangu, wanajaribu uelewa wangu wang’amue uhambe wangu. Tena kwa kweli si rahisi kujibu kila swali unaloulizwa.

Mpwa wangu wa kike juzi alipewa na babaye arafa ya simu iliyoandikwa na mdogo wake yule mpwa kumuumbua baba yao. Ilikuwa arafa ndefu inayoorodhesha na kufafanua adha anazomletea mama baba yao.

Baba alikasirika sana kuumbuliwa na mwanawe. Alitaka kujua maoni ya mpwa wangu huyu kuhusu arafa. Alipomaliza kuisoma, baba alimuuliza, “unaonaje hii arafa?”

Kwa ujuba au sijui ujuaji wake, akasema “nafikiri mdogo wangu alikuwa anajaribu kuwasilisha hisia zake.” Jibu hilo. Baba wa mtu alihamaki hadi ya kuhamaki. Akamfurusha bintiye maskanini: “Hapa usirudi tena.”

Nilitafakari kuhusu swali la mtu yule nisiyemfahamu. Nafikiri kuna maswali yanayostahiki kujibiwa na mengine yanayostahili kunyamaziwa.

Rafiki mwendazake Omar Babu ndiye aliyekuwa akisema jibu la mpumbavu sukuti, yaani ukiulizwa swali la kipumbavu mara nyingi huwa afadhali kunyamaza. Yesu Kristo, mtu mkuu zaidi aliyewahi kuishi hapa duniani, alitambua hilo.

Mara nyingine alipoulizwa maswali ya kihuni alinyamaza kimya (“hakukimya” kama watu wapendavyo kusema siku hizi “umekimya”)..

Nilipiga moyo konde kumjibu muulizaji na liwe liwalo. Nikamwambia kwa njia ya arafa ya simu kwamba mtu aliyeajiriwa na magereza kutekeleza hukumu ya kifo anaitwa “chakari.”

Muulizaji alifurahi sana kama alivyoeleza katika arafa yangu. Alikuwa mwingi wa shukrani. Nikafurahi kwa kutoa; kama msemo wa hekima usemavyo; “kuna furaha zaidi katika kutoa kuliko katika kupokea.”

Nilihisi hasara yangu kwa wengine kwa kushindwa au kukataa kuwajibu baadhi ya waulizaji wangu.

Kumbe huwa najikosesha tija. Labda wanaouliza maswali ya lugha na fasihi si watu wa kunyamaziwa, ni wasaka-maarifa, nami kama naweza nawajibika kuchangia mafanikio ya msako wao.

Ila kwa kweli mimi mwenyewe msakaji, nasaka maarifa siku zote. Nami pia nina maswali mengi ambayo huwa ninawauliza watu wengine, sio kwa lengo la kutaka kuwatega au kuwaweka kwenye mizani, hata kidogo. Sina matilaba wala hulka ya aina hiyo.

Mathalan, kama Mwalimu Enock Bitugi Matundura alivyobainisha katika makala ya wiki iliyopita, niliuliza wenzangu nini “case study” katika Kiswahili.

Swali langu lilizua midahalo mikali muhimu kuhusu istilahi na msamiati, kuhusu uhuru wa mwanataaluma kubuni istilahi na haki ya taaluma kuwa na usawazishaji na usanifishaji wa istilahi, kuhusu tofauti za istilahi za mwanataaluma huyu na yule, chuo hiki na kile na nchi hii na ile.