KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kila kitu kinakuja na kupita lakini maisha lazima yaendelee

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kila kitu kinakuja na kupita lakini maisha lazima yaendelee

NA WALLAH BIN WALLAH

NDUGU wapenzi imenibidi kumnukuu Dkt. Robert Schuller Mwandishi maarufu wa vitabu vya Kiingereza aliyeandika vitabu viitwavyo Tough Times Never Last , But Tough People Do (1988)! Pamoja na: Success is Never Ending, Failure is Never Final (1989)!

Katika kitabu cha kwanza Dkt. Schuller anatwambia kwamba, “Nyakati ngumu hazidumu; huja na kupita! Lakini watu wagumu wavumilivu hubakia pale pale wakiendelea na maisha yao baada ya kupitia na kupitiwa na nyakati ngumu za dhiki na mashaka!”

Sisi sote tunaelewa jinsi wananchi wa Kenya walivyopitia wakati mgumu wa hekaheka za kampeni na hamkani za kunadi sera kutoka kwa waaniaji uongozi kote nchini kwa mbwembwe na vurumai ungedhani dunia ingefikia kiyama!

Tumshukuru Mungu kutujalia kuwa wagumu na wavumilivu tukasalia salama baada ya wakati huo mgumu kupita!

Katika kitabu cha pili Mwandishi Dkt. Schuller anasema kwamba kufanikiwa sio mwisho wa kuendelea kuyasaka mafanikio zaidi. Aidha, kufeli au kushindwa nako sio mwisho wa kujitahidi kupambana tena na tena kutafuta kufaulu na kufanikiwa maishani ilimradi tu usikate tamaa!

Katika maisha kila kitu duniani kinakuja kinapita kinaenda. Na vinginevyo huja tena vikaenda! Ukipata shukuru! Na uendelee kutafuta zaidi! Pia ukikosa au ukishindwa kufanikiwa, usikate tamaa! Ujizatiti tu kutafuta tena siku nyingine! Hivyo ndivyo mambo yalivyo katika uchaguzi wa kusaka kura kukamia uongozi nchini! Kuna kupata na kukosa! Lakini maisha lazima yaendelee! Vumilia tu!

  • Tags

You can share this post!

Vurugu zatatiza shughuli ya kujumlisha kura Malindi

Washirika wa Uhuru waangushwa na Ruto

T L