KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Ukikataa kubadilika ujue kuwa mabadiliko ambayo yanatokea maishani ndiyo yatakubadilisha

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Ukikataa kubadilika ujue kuwa mabadiliko ambayo yanatokea maishani ndiyo yatakubadilisha

NA WALLAH BIN WALLAH

USIPIGANE wala kupingana na mabadiliko maishani!

Mabadiliko ni sehemu ya maisha duniani. Kila kitu kinapobadilika, wewe pia ubadilike na ubadilishe msimamo wako. La sivyo, mabadiliko yayo hayo yatakubadilisha!

Duniani tunaishi kwa mabadiliko katika matendo, mazingira, nyakati, tabia, mahitaji, uongozi, siasa, utamaduni, uchumi, hali ya anga na itikadi zetu.

Kila kitu kinabadilika.

Mabadiliko yote haya yanapotokea hubadilisha hadi utaratibu wa kuishi na kusababisha mfumko wa bei za bidhaa adhimu wanazozitumia wanadamu ulimwenguni.

Wakati wowote unapoyaona mabadiliko yakibisha hodi, uwe tayari kubadilika ili usiachwe na wakati!

Tazama jinsi lugha ya Kiswahili ilivyobadilika tangu enzi za Wangozi wa Shungwaya, tukaja kwa mabingwa wa awali kama akina Muyaka Bin Haji na Sheikh Shaaban Robert mpaka kufikia leo kwa vijana wetu wa sasa wanaojishasha na kujivunia lugha yao ya sheng’!

Chunguza utafakari mikikimikiki ya kisiasa na uongozi katika nchi zetu tangu tupate uhuru enzi za Mzee Jomo Kenyatta, Mwalimu Kambarage Nyerere, Dkt Milton Apollo Obote.

Wakafuatiwa na Mzee Daniel Arap Moi, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Idi Amin Dada na wengineo hadi leo nchi zetu zinapoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda na Ndugu yetu hapa Kenya Dkt William Samoei Ruto. Mabadiliko mengi yametokea. Na bado yanazidi kutokea tu.

Hapo ndipo nimejuzika kukutanabahisha kwamba mabadiliko ni kimbunga cha maisha. Usipobadilika ujue mabadiliko yatakubadilisha ima fa ima. Badilika!

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Annette Odusi

Omanyala sasa alenga dhahabu ya Riadha za Dunia 2023 na...

T L