KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Ukitumia ubongo wako vizuri utapata mawazo mazuri ya kutenda mambo mazuri

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Ukitumia ubongo wako vizuri utapata mawazo mazuri ya kutenda mambo mazuri

NA WALLAH BIN WALLAH

KICHWA cha mwanadamu kimebeba na kuhifadhi ubongo ambao ndio humsaidia mtu kuwaza na kutambua mambo maishani.

Mawazo ya mtu yaliyotengenezwa katika ubongo yanapotamkwa huwa maneno ambayo yakinenwa na kutendwa hubadilika kuwa matendo! Ubongo hubuni mawazo yanayokuwa maneno! Kisha maneno hugeuzwa kuwa matendo ambayo ndiyo matokeo halisi yanayoonekana kwa macho!

Ni muhimu kutumia ubongo kwa makini sana. Ni muhimu zaidi mtu ayatoe mawazo yake kwa uangalifu, busara na uadilifu mkubwa! Ukiyasema maneno bila umakinifu wala kufikiri utakuwa umeropoka na kupayuka badala ya kunena! Mwenye busara hutahadhari kabla ya kusema!

Ukweli ni kwamba ukiwaza vizuri kisha uyatamke mambo uliyoyawaza na uyatekeleze vyema, bila shaka utakuwa umeacha sifa na matendo mema yatakayokumbukwa duniani. Epuka kusema maneno duni wala usiyatende matendo yatakayokuaibisha na kukujutisha maishani! Waza vizuri na useme vizuri maneno yanayoweza kuwavutia watu hadi watamani kuiga ubora wako, fikra zako na matendo yako.

Ndugu wapenzi, maneno yanaweza kujenga na kubomoa nchi! Jitahidi zaidi kutumia ubongo vizuri kuwaza mawazo na matendo mazuri yanayosaidia kujenga nchi na wananchi wote!

Toa ushauri na mawaidha ya busara! Mawaidha ya hekima yakitolewa kwa heshima na maarifa yataleta ari na hamasa ya kuendeleza nchi na kuwaunganisha wananchi wote! Huo ndio msingi bora wa ubora wa mwanadamu anayetumia ubongo wake vizuri kuleta mafanikio na maisha mema duniani.

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Umuhimu wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili...

Shirikisho kuandaa vipute vingi kunoa Wapwani katika magongo

T L