Lugha, Fasihi na Elimu

KAULI YA WALLAH: Harakati za kila mwanadamu ni kutafuta jinsi ya kuishi vizuri duniani

February 28th, 2024 1 min read

Na WALLAH BIN WALLAH

TUSISAHAU na kujisahau kwamba shida ni nyingi kuliko furaha za dunia. Furaha ni chembechembe ndogo ukilinganisha na mapande makubwa makubwa ya mateso. Kwa hivyo jiweke tayari utapokabiliana na matatizo hayo.

Matatizo yapo kila kunapokucha. Wala hatuwezi kuyatatua matatizo kwa kuyatumia matatizo.

Kila tatizo hufuatwa na tatizo. Tunaishi katika shida bin shida. Lakini hayo yasikukatishe tamaa. Ajabu ni kwamba kila mtu ana safari yake ya kuyasaka maisha. Ole wetu katika safari hiyo ya pamoja kwenye msafara wa kusaka tonge, hatufiki kwa wakati mmoja.

Aidha hatutapata riziki na bahati zinazofanana. Kila mtu ana majaliwa yake. Ujue hivyo!

Panapotokea kwamba sisi sote hatujafanikiwa kwa namna zinazofanana, hapo ndipo tutumie ubongo na akili zaidi. Ujifunze na kufikiria utafanya nini na usifanye nini? Usipotumia akili unaweza kudhania Mungu hakupendi.

Ati anawapendelea wengine. Mungu ni Mungu tu! Usipotumia akili komavu unaweza kutawaliwa na wivu hadi utamani kumwangamiza aliyefanikiwa.

Uamuzi kama huo utakuongezea nini? Ukiamua kumchukia na kumuadhibu kwa kumwangamiza utafaidika vipi? Tumia mafanikio ya wenzako kama kigezo au kielelezo cha wewe pia kufanikiwa ili labda upige hatua kama yeye au zaidi yake.

Lazima tukubali kwamba kupata na kukosa ni majaliwa. Wazembe zaidi duniani baada ya kushindwa kufanikiwa kama fulani hufikia hatua ya kujiangamiza wao wenyewe. Utakuwa umeacha funzo gani duniani?