Kauli za Uhuru zatishia Raila

Kauli za Uhuru zatishia Raila

Na BENSON MATHEKA

KAULI za Rais Uhuru Kenyatta kwa wafuasi wake eneo la Mlima Kenya kwenye chaguzi za 2013 na 2017, zinatishia juhudi zake za kumpigia debe kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga katika eneo hilo.

Wakati wa kampeni hizo, Rais Kenyatta alimsawiri Bw Odinga kama mtu hatari kwa maslahi ya wakazi wa eneo hilo akimtaja kama muguruki au kimundu, kauli ambazo imekuwa vigumu kwake kufuta.

Kwenye kampeni hizo, Rais Kenyatta alikuwa akiwaahidi wafuasi wake kwamba chama cha Jubilee kingetawala kwa miaka 20 akisema yeye angetawala kwa miaka 10 kisha amuunge naibu wake Dkt William Ruto kutawala kwa miaka mingine 10.

Alimsawiri Bw Odinga kama mtu asiyeweza kuaminiwa akimpaka tope ili wapigakura wamkatae na kumchagua yeye pamoja na Dkt Ruto.

Baada ya handisheki yake na Bw Odinga mnamo Machi 2018, Rais Kenyatta alianza kumsifu Bw Odinga, hatua ambayo ilizua mgawanyiko katika ngome yake ya Mlima Kenya na katika chama cha Jubilee.

Ingawa amekuwa akisema kuwa yeye na Bw Odinga walizika tofauti zao mnamo Machi 8, 2018 na kuanza kujenga daraja la maridhiano, ameshindwa kuwashawishi wakazi wa eneo la Kati kwamba waziri huyo mkuu wa zamani amekuwa ‘malaika’ wanayestahili kukumbatia.

Jinsi ushirikiano wake na Bw Odinga unavyokita mizizi na kuonekana kama chaguo la mrithi wake, ndivyo wakazi wa Mlima Kenya wanavyoendelea kumuasi. “Wapi kumi ya Uhuru na kumi ya Ruto,” washirika wa Dkt Ruto eneo hilo wamekuwa wakiuliza.

“Ni rais mwenyewe aliyesema hadharani kwamba ataongoza kwa miaka 10 na kisha Ruto atuongoze kwa miaka mingine 10. Ni ahadi hiyo inayotufanya kumuunga Dkt Ruto,” asema mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome.

Rais Kenyatta ameshindwa kushawishi wakazi wa eneo la Mlima Kenya kuacha kumuunga Dkt Ruto licha ya kumsawiri kama fisadi. Hii ilidhihirika chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho Dkt Ruto amejihusisha nacho baada ya kutengwa serikalini kilipobwaga chama cha Jubilee kwenye chaguzi ndogo sita eneo la Mlima Kenya.

“Imekuwa vigumu kwa Rais Kenyatta kufuta kauli ya ‘yangu kumi na kumi ya Ruto’. Ameshindwa pia kushawishi wakazi kwamba Bw Odinga si mchawi alivyowafanya kuamini wakati wa uchaguzi mkuu uliopita,” asema mdadisi wa siasa Timothy Muriuki.

Inasemekana kuwa mikakati ambayo Rais Kenyatta amekuwa akibuni kumpenyeza Bw Odinga eneo la Mlima Kenya imekuwa ikigonga mwamba wakazi wakisema hawapi sababu za kuridhisha za kutomuunga Dkt Ruto.

Kulingana na mbunge mmoja anayeunga handisheki ambaye alizungumza nasi kwa sharti kuwa tusimtaje jina, mbinu ya hivi punde ilikuwa kutumia wanamuziki ambao Rais Kenyatta alitumia kutunga nyimbo za kumkashifu Bw Odinga kuanzia 2013.

“Hafla ya wanamuziki ambayo tulihudhuria Murang’a juzi Bw Odinga akiwa mgeni wa heshima ilikuwa mbinu ya kutaka kusafiana nia na wasanii hao ambao wana ushawishi mashinani. Hii ni kwa sababu imekuwa vigumu kutumia wanasiasa ambao wamegawanyika,” asema mbunge huyo.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanasiasa wanaounga handisheki wakiwemo wabunge na magavana ambao waliahidi kumpigia debe Bw Odinga eneo la Mlima Kenya.

Ingawa amekuwa akimsifu Bw Odinga na kuahidi kushirikiana naye siku zijazo, Rais Kenyatta hajawahi kuandamana na kiongozi huyo wa upinzani kwa ziara ya kisiasa au maendeleo eneo la Mlima Kenya, hatua ambayo Bw Muriuki anasema inatokana na kushindwa kufuta matamshi yake kumhusu wakati wa kampeni.

You can share this post!

Ziara ya Rais eneo la Magharibi yayumba

Hatimaye Moi atangaza kuwania urais 2022