Kauli za ‘wafia Ruto’ zinavyopunguza ufuasi wake Mlimani

Kauli za ‘wafia Ruto’ zinavyopunguza ufuasi wake Mlimani

NA WANDERI KAMAU

UUNGWAJI mkono wa Naibu Rais William Ruto uko hatarini katika eneo la Mlima Kenya, kufuatia kauli za baadhi ya washirika wake Jumamosi iliyopita katika Kaunti ya Uasin Gishu, zilizoonekana kuzilenga jamii za Mlima zinazoishi katika Bonde la Ufa.

Baadhi ya washirika wake waliotoa kauli hizo tata ni maseneta Mithika Linturi (Meru), Aaron Cheruiyot (Kericho) kati ya viongozi wengine.

Ijapokuwa Dkt Ruto tayari ameomba radhi kuhusiana na matamshi hayo na hata kuwarai washirika wake kuwa waangalifu wanapowahutubu kwenye mikutano ya kisiasa, kumeibuka hofu mpya katika eneo hilo kuwa “Dkt Ruto si rafiki wa kweli” wa wenyeji kama ambavyo amekuwa akijisawiri.

Wenyeji, viongozi na wadadisi wa siasa wanasema Dkt Ruto alifanya kosa, ambalo huenda ikawa vigumu sana kulirekebisha.

Tayari, Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) imeanza kuchunguza baadhi ya wanasiasa.

“Licha ya Dkt Ruto kuomba radhi kuhusu kauli hizo, zinaturejesha katika miaka ya tisini, wakati ghasia za kikabila zilichipuka na kuchacha katika eneo la Bonde la Ufa. Ashaharibu msingi uliokuwepo. Itakuwa vigumu kwake kurejesha ufuasi mkubwa aliokuwa nao katika eneo la Mlima Kenya licha ya kuomba msamaha,” akasema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za Kati.

Kulingana na mchanganuzi huyo, neno “madoadoa” lilizua hofu kuanzia mwaka 1992, kwani lilitumiwa na wanasiasa katika eneo hilo kuwaagiza wenyeji kuwafurusha watu wanaotoka katika maeneo mengine nchini.

Anasema ni neno lililovuruga uthabiti na mshikamano wa kisiasa uliokuwepo katika eneo hilo kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

“Hata ikiwa Bw Linturi na wanasiasa wengine walifafanua muktadha uliowasukuma kutumia neno hilo, maji yashamwagika. Kilichobaki ni mlima mkubwa sana kwa Dkt Ruto kuukwea ili kurejesha ufuasi aliokuwa nao awali Mlima Kenya,” akasema Prof Njoroge.

Wenyeji kadhaa waliozungumza na ‘Jamvi la Siasa’ walitoa kauli kama hizo, wakisema matamshi hayo yalionyesha kuwa vidonda na ghasia za kikabila zilizoshuhudiwa kati ya 1992 na 2007 bado vingali hai.

“Kile washirika wa Dkt Ruto walisahau ni kuwa moja ya athari za ghasia za 2007 ni kubuniwa kwa serikali ya Jubilee kutokana na kesi zilizowakabili Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), mjini The Hague, Uholanzi. Walisahau pia undani wa mzozo huo ni tofauti za kisiasa baina ya maeneo ya Mlima Kenya na Bonde la Ufa,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wadadisi wanasema ikiwa Dkt Ruto hatachukua hatua za haraka, basi ‘kosa’ hilo la kisiasa litampa mwanya kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kuimarisha mpenyo wake wa kisiasa Mlimani.

Wanasema ingawa bado ufuasi wa Dkt Ruto ni mkubwa ikilinganishwa na Bw Odinga, kuna uwezekano mkubwa (Bw Odinga) kupenya kisiasa eneo hilo kupitia vuguvugu la Azimio la Umoja, ambalo kaulimbiu yake kuu ni umoja na utangamano miongoni mwa jamii mbalimbali nchini.

Mwezi Oktoba 2021, Dkt Ruto alidai “kulimiliki kisiasa” eneo la Mlima Kenya, akimwonya Bw Odinga na washirika wake “kupitia kwake” ikiwa wanatafuta uungwaji mkono wa kisiasa kutoka kwa wenyeji.

Wadadisi wanasema kauli hiyo ya Dkt Ruto ilitokana na imani kubwa aliyokuwa nayo kuwa hakuna kigogo yeyote wa kisiasa ambaye angetikisa umaarufu wake.

“Kando na ahadi za kuboresha masuala kama uchumi, afya na elimu, ahadi kuu ya Bw Odinga imekuwa ni kurejesha umoja wa nchi. Ni mkakati ambao huenda Bw Odinga akatumia kujizolea ufuasi katika maeneo ambayo Dkt Ruto alikuwa ashajizolea umaarufu wa kisiasa,” asema mdadisi wa siasa, Bw Wycliffe Muga.

  • Tags

You can share this post!

Wakulima warai Munya aingilie kati kuhusu deni

Mlima wabusu Raila

T L