Habari Mseto

Kauli zatolewa kuhusu BBI

October 25th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

BAADA ya ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) kuzinduliwa rasmi siku chache zilizopita, viongozi na wananchi wameanza kutoa maoni yao kuihusu.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wanaina, alitoa ushauri kwa kila Mkenya popote alipo awe mstari wa mbele kujisomea ripoti hiyo ya BBI.

“Ninahimiza Wakenya waketi chini na kujisomea wenyewe bila kutegemea yeyote na iwapo wataichangamkia bila shaka wana nafasi njema ya kuipitisha. Lakini kama hawaipendi basi waikatae na tuendelee mbele,” alisema Bw Wainaina.

Aliwataka wananchi wasikubali kupotoshwa kuhusu ripoti hiyo lakini wawe makini na wajisomee wenyewe bila kushinikizwa.

Aliyasema hayo mnamo Jumamosi alipohutubia wakazi wa mji wa Thika wakati akiwashauri kuhusu ripoti hiyo.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika, Bw Alfred Wanyoike, pia alifuata mwito huo wa mbunge huyo kwa kuwashauri wananchi wawe mstari wa mbele kusoma ripoti hiyo.

“Tunafurahia kuhusu maswala ya vijana ambao wamepewa muda kufanya kazi ili walipe mikopo yao baadaye. Hiyo itawapa mwelekeo mzuri wa kujipanga vyema,” alisema Bw Wanyoike.

Pia alipendekeza ripoti hiyo iandikwe kwa lugha rahisi itakayoeleweka upesi.

Hata majukumu ya naibu gavana yameangaziwa kwa njia mwafaka, alisema.

“Kwa hivyo tunaonelea baadhi ya mambo yaliyo ndani ya BBI ni ya kuleta matumaini. Kwa hivyo hakuna haja ya kuchukia mwenzako kwa sababu ya ripoti hiyo,” alisema Bw Wanyoike.

Bw Frankline Mugambi ambaye ni mkazi wa Thika alisema watu wengi walikuwa wameingoja ripoti hiyo kwa hamu na kwa hivyo kila mmoja ana nafasi ya kuisoma mwenyewe.

Alisema kama ripoti hiyo itamfaa mwananchi bila shaka inastahili kupitishwa haraka.

“Tungetaka ufisadi uangamizwe kupitia ripoti hiyo. Hatungependa mgawanyiko wowote bali ni vyema ripoti hiyo iunganishe Wakenya wote,” alisema Bw Mugambi.

Alisema iwapo litamfaidisha mwananchi kikamilifu bila shaka kila mmoja atakuwa mstari wa mbele kuipitisha.

“Sisi kama wananchi hatungetaka kushurutishwa na yeyote kuhusu ripoti hiyo kwa sababu tunataka tujiamulie wenyewe. Kwa hivyo ningewasihi wananchi popote walipo wawe watu wa kwanza kuisoma kikamilifu,” alisema Bw Mugambi.

Alisema ripoti hiyo imeangazia mazuri kwa vijana ambao wanaonekana watajipanga vyema kwa muda fulani ili kulipa mikopo yao.