Kaunti 10 za Mt Kenya kuondoa ada za biashara

Kaunti 10 za Mt Kenya kuondoa ada za biashara

Na JAMES MURIMI

MUUNGANO wa Kiuchumi wa Kaunti za Eneo la Kati (CEREB) umeanza kubuni mkakati utakaounganisha ada zinazotozwa mipakani, ili kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati yao.

Mkakati huo pia utaondoa vikwazo vingine ambavyo vimeathiri shughuli za kibiashara za kaunti hizo.

Tayari, maafisa wakuu wa CEREB wameanza vikao vya siku mbili mjini Nanyuki kujadili namna ya kubuni soko la pamoja, litakalowaondolea wafanyabiashara mzigo wa ada nyingi wanaposafirisha bidhaa kutoka kaunti moja hadi nyingine.

Muungano huo unashirikisha kaunti kumi ambazo ni Laikipia, Meru, Kiambu, Nakuru, Murang’a, Nyandarua, Embu, Kirinyaga, Tharaka Nithi na Nyeri.

Kilimo ndicho kitegauchumi kikuu cha kaunti hizo. Baadhi ya ada zinazolengwa ni malipo ya kusafirisha bidhaa, utengenezaji bidhaa na masoko.

Kaunti hizo zinatarajiwa kubuni mkataba ambao utaondoa baadhi ya malipo ya leseni kwa watengenezaji bidhaa na watoaji huduma mbalimbali.

Ili kupunguziwa ada hizo, lazima shirika ama mfanyabiashara husika athibitishe anatoka katika moja ya kaunti hizo kumi.

Akiwahutubia wanahabari Alhamisi, mwenyekiti wa Jopo Maalum la Kibiashara la muungano huo, Bi Diana Kendi, alisema kuwa wanatathmini kwa kina sababu ambazo zimekuwa zikiathiri ustawi wa biashara katika eneo hilo.

“Mapato ya jumla ya kifedha ya eneo hili ni ya juu ikilinganishwa na baadhi ya nchi duniani. Hiyo ndiyo sababu tunaangalia njia za kuimarisha biashara miongoni mwetu, ili kujiweka pazuri kushirikiana kibiashara na maeneo mengine ya kanda,” akasema Bi Kendi.

“Tuliona kukiwa na vikwazo vingi katika usafirishaji wa bidhaa kama maziwa kutoka eneo moja hadi jingine kutokana na ada nyingi zinazotozwa. Sekta hiyo haijakuwa ikifanya vizuri na wakulima hawajakuwa wakupata faida kubwa. Tunaweza kubuni njia za kujipatia mapato bila kuwahangaisha wafanyabiashara,” akaongeza Bi Kendi, aliye pia Waziri wa Biashara katika Kaunti ya Nyeri.

Kikao hicho kilianza Alhamisi. Mkutano ulihudhuriwa na magavana wote kumi kutoka eneo hilo.

Muungano huo pia umekuwa ukipata uungwaji mkono kutoka kwa Wizara ya Biashara na Viwanda nchini.

“Tunawashukuru magavana wetu kwa kutuongoza kuandaa kikao hiki. Tutatuma maamuzi makuu kwa magavana ili wayapitishe rasmi,” akasema Bi Kendi.

“Ikiwa una leseni ya kuendesha biashara yako ya kutengeneza bidhaa katika Kaunti ya Kiambu, hutahitajika kulipia ada ya kuzisambaza katika Kaunti ya Nakuru ama kaunti yoyote ambayo ni mwanachama wa muungano huu,” akongeza Bw Githuku Mungai, ambaye ni mshauri kwa Serikali ya Kaunti ya Laikipia.

You can share this post!

Wizara yakosa kutaja hesabu kamili ya fedha zilizotumika...

Kalonzo arai Raila awe mgombea mwenza wake uchaguzini 2022