Kaunti 43 hazijatengea ‘Big 4 Agenda’, ripoti yasema

Kaunti 43 hazijatengea ‘Big 4 Agenda’, ripoti yasema

Na RUSHDIE OUDIA

UKOSEFU wa mipangilio ya ujenzi ni miongoni mwa changamoto kuu zilizolemaza utekelezwaji wa miradi mikuu minne ya Rais Uhuru Kenyatta katika kaunti 43, imebainika.

Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) pamoja na Wizara ya Ardhi zimeelezea wasiwasi kwamba nyingi ya kaunti nchini hazijatenga maeneo spesheli kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, nyumba na kuwekeza miradi ya kuzalisha chakula.

Ripoti ya NLC inaonyesha kuwa Kisumu ni miongoni mwa kaunti ambazo hazijatenga maeneo kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Ukosefu wa mpango wa ujenzi pia huenda ukatatiza kutengwa kwa eneo maalumu la kibiashara katika Kaunti ya Kisumu.

Lakini waziri wa Ardhi wa Kaunti ya Kisumu, Profesa Judith Atyang’, alijitetea kwa kusema kuwa wizara yake inakaribia kukamilisha maandalizi ya mpango wa ujenzi.

“Tumekaribia kukamilisha shughuli ya kupanga ujenzi jijini. Mpango huo ukikamilika utatoa mwonekano mpya jijini. Tumeanza kuondoa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiuza bidhaa zao kwenye maeneo yasiyofaa katikati mwa jiji,” akasema.

Kaunti nyingine ambazo hazijatenga maeneo ya kibiashara ni Homa Bay, Nyamira, Migori, Busia, Kisii, Kakamega, Vihiga, Garissa, Elgeyo Marakwet na Turkana.Nyingine ni Narok, Taita Taveta, Machakos, Mandera, Meru, Embu, Tharaka Nithi na Isiolo.

Mwenyekiti wa NLC Gershom Otachi na kamishna Esther Murungi walisema kuwa ni kaunti nne pekee zilizo na mpango wa ujenzi.Kaunti zilizo na mipango ya ujenzi iliyoidhinishwa na mabunge ya kaunti ni Lamu, Makueni, Baringo na Kericho.

Kaunti ambazo zimekaribia kukamilisha upangiliaji wa ujenzi ni Siaya, Kajiado, Nyeri, Kirinyaga, Kwale, Murang’a, Uasin Gishu na Nyandarua.

Bw Otachi alisema miji inayoibuka kama vile Mlolongo, Syokimau, Kitengela na Ongata Rongai haina mipango ya ujenzi – hali ambayo inasababisha wawekezaji kujenga kiholela.

“Kaunti tulizozungumza nazo zinadai kuwa hazina fedha za kuandalia fedha za ujenzi,” akasema Bw Otachi.

Maafisa hao wa NLC walikuwa wakizungumza mjini Kisumu wakati wa ufunguzi wa warsha ya chama cha Wataalamu wa Upangiliaji wa Ujenzi wa Miji na Kaunti.

You can share this post!

WARUI: Kufeli kwa wauguzi kunaibua maswali kuhusu mfumo wa...

Jamaa wa Gumo aliyetekwa nyara aachiliwa

T L