Kaunti kuadhibu ‘makanjo’ dhalimu

Kaunti kuadhibu ‘makanjo’ dhalimu

Na COLLINS OMULO

BUNGE la Kaunti ya Nairobi limeanzisha uchunguzi kwa lengo la kuwanasa maaskari – maarufu kama kanjo – ambao wamekuwa wakijihusisha na visa vya dhuluma jijini.

Uchunguzi huo unafuatia ripoti kuwa askari wa kanjo alishambulia pasta wa Kanisa la Anglikana (ACK), Jumatano.Mnamo Julai, mwaka huu, maafisa watatu wa kanjo walijipata pabaya baada ya kumpiga na kumng’oa meno matano Anthony Maina ambaye ni mchuuzi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Sheria wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Joseph Komu, alisema madiwani wataanzisha uchunguzi kwa lengo la kuwachukulia hatua kali kanjo ambao wamekuwa wakiwahangaisha watu jijini.

“Tumebaini kuwa kuna shida jijini na sasa tumeamua kuanzisha uchunguzi kubaini kiini. Maafisa watakaopatikana na hatia watawajibishwa,” akasema Bw Komu. Malalamishi dhidi ya kanjo yaliwasilishwa bungeni na diwani wa Nairobi South, Waithera Chege.

ambaye alisema kuwa maaskari hao wamekuwa wakidhulumu wachuuzi na wafanyabishara wengine jijini.Naibu kiranja wa wengi huyo alisema kuwa kanjo wanaotekeleza uovu huo hawajakuwa wakiadhibiwa hata baada ya kuripotiwa.

“Uovu wa aina hiyo haufai kufumbiwa macho; wahusika ni sharti waadhibiwe,” akasema Bi Chege.Diwani wa Woodley, Mwangi Njihia, alisema kuwa: “kanjo wamekuwa hatari jijini kwani wamekuwa wakidhulumu hadharani wahudumu wa bodaboda na wachuuzi wanaokataa kutoa hongo.”

You can share this post!

Simu 2 zilizotupwa na magaidi waliotoroka Kamiti zapatwa...

Wadhifa wa Mwakilishi wa Kike Kaunti wakosa kuvutia...

T L