Habari Mseto

Kaunti kubomoa vibanda kando ya barabara

October 21st, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Kaunti ya Garissa imetoa ilani ya siku saba kwa watu waliojenga vibanda katika ardhi ya umma kando ya barabara mjini Garissa, waviondoe la sivyo vibomolewe na wahusika kuchukuliwa hatua.

Akiongea wakati wa Sherehe za Mashujaa Dei, Gavana wa Kaunti hiyo, Bw Ali Korane, alisema unyakuzi wa ardhi ni uovu ambao umesababisha vita na maafa katika mji huo.

Uovu huo, alisema, umekuwa ukiendelea licha ya serikali yake na ile ya kitaifa kutoa onyo dhidi ya unyakuzi wa ardhi.

“Tumetoa notisi hii ya siku saba ili wenye vibanda hivi waviondoe. Wasipotii notisi hii watafurushwa kwa nguvu kando na kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” akasema Bw Korane.

Gavana huyo pia aliwakashifu baadhi ya wanasiasa wa kaunti hiyo aliosema wamekuwa wakieneza chuki na uhasama huku wakichochea wananchi dhidi ya serikali yake.

Bw Korane aliwataka kukomesha siasa chafu na badala yake waendeleze masuala ambayo yanaweza kuchochea maendeleo katika kaunti.