Kaunti kupokonywa chanjo zipelekwe kwingine

Kaunti kupokonywa chanjo zipelekwe kwingine

Na IRENE MUGO

KAUNTI ambazo zina idadi kubwa ya watu wanaosusia chanjo ya virusi vya corona, zitapokonywa chanjo hizo ili zipelekwe kaunti nyingine zinazozihitaji.

Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe alisema Ijumaa kuwa kuna takriban dozi 200,000 za chanjo ya AstraZeneca ambazo hazijatumiwa nchini.

“Tutatwaa dozi za chanjo kutoka kwa kaunti ambapo utoaji chanjo unafanyika polepole mno. Hatuwezi kuacha zipitwe na muda wa matumizi yake. Tutazisambaza kwingineko,” akasema Bw Kagwe.

Hata hivyo, hakufichua ni kaunti gani zitakazopokonywa chanjo.

Alikuwa akizungumza Ijumaa katika Kaunti ya Nyeri wakati wa uzinduzi wa mataneti katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), tawi la Othaya.

Kwa mujibu wa takwimu alizotangaza Bw Kagwe, idadi ya watu waliopokea chanjo kufikia Ijumaa ilikuwa ni 911,515. Serikali ilikuwa imepokea dozi 1.2 milioni.

Miongoni mwao, watu 531,540 ni wenye umri wa zaidi ya miaka 58, wahudumu wa afya 160,468, walimu 142,624 na maafisa wa usalama 76,578.

Takwimu hizo zinadhihirisha kuwa, licha ya wito uliotanda kutaka watu wanaotoa huduma muhimu wapewe chanjo kwanza kabla ya wananchi wengine, wengi wao wamekataa kujitokeza.

Kuhusu aina mpya ya virusi vya corona kutoka India, Bw Kagwe alisema serikali imefanikiwa kuidhibiti ili isienee zaidi.

Aina hiyo ya virusi ambayo ni hatari na inasambaa kwa kasi kuliko aina nyinginezo, ilikuwa imepatikana kwa watu ambao walisafiri kutoka India hadi Kisumu hivi majuzi.

Watu 568 Ijumaa walithibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Hukumu ya Zakatul Fitr na namna ya...

Serikali yasisitiza kufungua shule Jumatatu