Kaunti kutoa ardhi zaidi kwa ajili ya upanzi wa kahawa

Kaunti kutoa ardhi zaidi kwa ajili ya upanzi wa kahawa

NA GERALD BWISA

UTAWALA mpya wa kaunti ya Trans Nzoia umeunga mkono mipango ya kuongeza ardhi ya upanzi wa Kahawa kwa wingi.

Gavana George Natembeya alibainisha kuwa kaunti yake ina uwezo mkubwa wa kustawi katika kilimo cha zao hilo.

Bw Natembeya amefichua mipango ya utawala wake kuongeza ardhi inayozalishwa kahawa kutoka 2,535 Ha hadi 10,000 Ha ifikapo mwaka 2023.

Mnano Jumamosi, wakati wa sherehe za kimataifa za Siku ya Kahawa 2022, Bw Natembeya alisema utawala wake umejitolea kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Zaidi ya hayo, aliongeza kwamba anatarajia kuona wakulima katika eneo hilo wakipanua wigo wao wa mapato.

Bw Natembeya alizungumza hayo katika Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Kahawa cha Muroki katika kaunti ndogo ya Saboti.

Gavana huyo ambaye alikuwa Mkuu wa Ukanda wa Bonde la Ufa alisema mahitaji ya kahawa yamekuwa yakipungua kwa miaka mingi kutokana na bei duni.

“Kwa hakika kaunti ya Trans Nzoia haiwezi kuorodheshwa miongoni mwa kaunti zenye uzalishaji mdogo wa kahawa wakati tuna uwezo wote. Ni lazima sote tung’ang’ane kupeleka kaunti hii mahali inapostahili kuwa,” akasema.

Akiahidi kuiomba serikali ya kitaifa kutoa ruzuku zaidi kwa gharama ya mbolea na pembejeo za kilimo, aliwasihi wakulima katika kaunti hiyo kukumbatia upanzi wa mimea mbalimbali.

Kando na hayo, aliwaomba pia, kuzingatia uzalishaji ili kupata faida ndiposa wakidhi mahitaji.

Bw Natembeya alitoa wito wa kuondolewa haraka kwa vizuizi ambavyo kwa muda mrefu vimewazuia wakulima kupata faida kubwa kutokana na zao hilo.

Alitaja, miongoni mwa mambo mengine, kukosekana kwa kanuni zinazofaa ambazo alisema, zimetoa mwanya kwa wafanyabiashara wa kati kuwanyonya wakulima wanaofanya kazi kwa bidii.

Aliongeza kwamba sababu hiyo inasababisha kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo ambalo hapo awali lilikuwa linaongoza kwa kuletea nchini ya Kenya pesa nyingi.

“Utawala wangu umejitolea kutoa mafunzo kwa wakulima juu ya mbinu bora za kilimo na uendelevu pamoja na kuwajengea uwezo wa kuwafanya wakulima wa kilimo,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Kilimo, Ushirika na Mifugo, Bi Mary Nzomo alisema idara yake inatekeleza mpango wa upanuzi wa mazao ili kupunguza hatari zinazohusiana na kutegemea zaidi uzalishaji wa mahindi.

Chini ya mpango huo, serikali ya kaunti inasisitiza kilizo cha ndizi, kahawa, chai, parachichi, makadamia na tufaha.

“Wakulima wanakabiliwa na uzalishaji duni na tija, uongezaji thamani duni, gharama ya juu ya uzalishaji, soko finyu, athari mbaya za mabadiliko ya hali ya anga na ukosefu wa mikopo nafuu na miundombinu na ndio maana serikali ya kaunti iko mbioni kushughulikia masuala hayo,” Bi Nzomo akasema.

Pia alijutia mizozo kati ya wanachama wa vyama vya ushirika ambayo alisema, imetatiza uzalishaji.

  • Tags

You can share this post!

Mulembe imani tele Mudavadi atawakwamua

Gachagua aendeleza kauli za kukanganya

T L