Kaunti lawamani kuhusu ubomoaji

Kaunti lawamani kuhusu ubomoaji

WINNIE ATIENO na FARHIYA HUSSEIN

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imelaumiwa kwa ubomoaji majengo ambao ulitokea katika sehemu tofauti za mji huo.

Katika kisa cha kwanza, mfanyibiashara anayemiliki kampuni ya uokaji mikate ya Fayaz, Bw Mohamed Ayub alikashifu utawala wa Gavana Hassan Joho kwa kusimamisha miradi yake katika ufuo wa Bahari Hindi.

Kisa kingine kinahusu ubomoaji wa kituo cha mafuta, ambacho kilidaiwa kuwa katika sehemu inayofaa kuwa ya ujenzi wa nyumba za Buxton Point.

Mradi huo unaendelezwa na kampuni ya mwanasiasa Suleiman Shahbal kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Mombasa.

Bw Ayub alishtumu serikali ya Kaunti kwa kusimamisha ujenzi wa msikiti wa Madhubaha katika eneo la Mji wa Kale, lakini serikali ya kaunti ikasisitiza ardhi hiyo ni ya umma.

Mvutano ulichipuka Bw Ayub alipoanza ujenzi wa msikiti huo serikali ya Kaunti iliposema kwamba ujenzi huo unahitilafiana na barabara ya ufuoni na shughuli za uvuvi.

Bw Ayub anaeleza kuwa aliamua kufanya ujenzi huo baada ya eneo hilo kubadilishwa kuwa maficho ya watumizi wa dawa za kulevya na walevi.

“Kila mtu anajua Madhubaha ni maficho ya watumizi wa dawa za kulevya na walevi ndio maana tukaamua kubadilisha mandhari ya eneo hilo kwa kulijenga. Lakini nahangaishwa sana, tumechoka! Tumekuwa kwenye biashara kwa zaidi ya miaka 100 na hatujawahi kupitia uonevu huu,” alisema Bw Ayub.

Alieleza kuwa anamiliki ardhi hiyo ingawa afisa wa uchukuzi na ujenzi katika Kaunti, Bw Tawfiq Balala alieleza kuwa ardhi hiyo haifai kumilikiwa na mtu binafsi.

“Fuo zote ni za umma, hazimilikiwi na watu binafsi. Hatupingi ujenzi wa msikiti jinsi inavyodaiwa,” alisema. Kwa miaka mingi, sehemu hiyo maarufu ya Madhubaha imekuwa ikitumiwa na wavuvi na watengenezaji wa boti. Wavuvi walimshtumu mfanyibiashara huyo kwa kutaka kuwafurusha.

Lakini Bw Ayub alisema hajakataza wavuvi kuendeleza biashara zao sehemu hiyo. Hata hivyo, Bw Balala alimtaka Bw Ayub kufanya kikao na serikali ya Kaunti kusuluhisha mgogoro huo.

Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini Kenya liliingilia mzozo huo na kutaka lisifanywe kuwa mzozo wa kidini.Wakazi pia wanalia kuhusiana na ubomozi wa kituo cha mafuta.

“Babangu alijenga kituo hiki cha mafuta miaka 20 iliyopita. Kamwe hakikuwahi kuwa na shida na serikali ya Kaunti mpaka sasa. Hatujapokea ilani yoyote au amri ya korti kwamba tunapaswa kuondoka katika eneo hili,” akasema mmiliki, Bi Najma Ahmed.

Alisema ubomoaji ulifanywa usiku wa manane wakapata mali zimeharibiwa Alhamisi asubuhi.Wakili wa familia, Bw Hassan Abdiaziz alisema wataelekea kortini ikiwa hawatapewa fidia.

Juhudi za kupata maoni ya serikali ya Kaunti kuhusu kisa hiki hazikufua dafu, lakini msimamizi mkuu wa mradi huo wa Buxton, Bw Ahmed Badawy alihimiza wenye malalamishi kuyawasilisha kwa serikali ya Kaunti.

You can share this post!

Shahidi apiga wakili ngumi kortini kwa kumuuliza swali

Ushawishi wa Kalonzo Pwani wafifia 2022 ikinukia