Habari Mseto

Kaunti ya Garissa kuwaajiri wahudumu wa afya maeneo yanayokabiliwa na upungufu

May 30th, 2020 1 min read

Na FARHIYA HUSSEIN

KAUNTI ya Garissa inapanga kuwaajiri maafisa wa afya kwa maeneo yanayokabiliwa na upungufu.

Akiongea katika ofisi yake, Katibu wa Kaunti hiyo Bw Abdi Ali alisema shughuli hiyo inalenga kuwasaidia wakazi ambao wanapitia wakati mgumu kupata huduma za afya kutokana na uhaba wa wafanyakazi.

Mbali na kuogeza maafisa wa afya ili kukabiliana na uhaba, kaunti hiyo imepokea vifaa kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali vile vya kusaidia kupambana na ugonjwa wa Covid-19.

“Tumepokea maski na glavu pamoja na vifaa vingine vya kujikinga (PPE) ili kuwasaidia maafisa,” akasema Bw Ali.

Bodi ya Huduma za Umma za Kaunti hiyo ndiyo inayosimamia shughuli ya kuwaajiri wafanyakazi wa afya.

Hulugho, Sangailu, Galmagala na Bura ni baadhi ya maeneo katika kaunti hiyo yanayokabiliwa na uhaba wa wahudumu wa afya.

Wiki moja iliyopita, wafanyakazi wa afya ambao walikuwa katika Hospitali ya Bura walihamishwa na polisi sababu kuu ikiwa kuhofia usalama wao, kushambuliwa na kundi la wapiganaji wa al-Shaabab. Ni hatua iliyowaacha wakazi wa eneo hilo bila huduma za afya.

Kamishna wa eneo la Kaskazini Mashariki, Nick Ndalana alisema ni uamuzi wa serikali kuhamisha wahudumu hao kuwapeleka pahala salama.

“Wafanyakazi wa afya hapo awali walihamishwa kutoka maeneo mengine na kupelekwa Bura. Ni shughuli ya kawaida kuhakikisha maisha ya wahudumu hao hayako hatarini,” Bw Ndalana alisema.

Walakini, uamuzi haukupokelewa vizuri na mbunge na wakazi wa eneo hilo.

Shirika la MUHURI linashirikiana na Serikali ya Kaunti ya Garissa kuhusu maswala ya dhuluma na ukatili.

Gavana wa Kaunti ya Garissa ni Ali Korane.