Kaunti ya Kilifi yaweka mikakati ya kuwashughulikia wagonjwa wa saratani

Kaunti ya Kilifi yaweka mikakati ya kuwashughulikia wagonjwa wa saratani

NA ALEX KALAMA

IDARA ya afya kaunti ya Kilifi imedokeza kuwa wagonjwa wa saratani wataanza kupokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya kaunti hiyo hivi karibuni.

Kulingana na mkurugenzi wa afya kaunti hiyo Hassan Hamisi, tayari mikakati imewekwa ili kuhakikisha vifaa vya matibabu ya ugonjwa huo vinapatikana.

“Katika hili jumba letu la Kilifi Medical Complex tunaingia awamu ya pili ambapo tutaimarisha kitengo cha kushughulikia wagonjwa wa saratani. Tutakuwa tukitoa huduma za chemotherapy na pia tutakuwa tunafanya screening katika hiki kituo chetu. Vilevile katika hospitali zetu tutaongeza vituo vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa hali ya juu bila kusahau wanaotafuta matibabu ya kupunguza madhara,” amesema Bw Hamisi.

Kubwa zaidi, Hamisi amesema kuwa hatua hiyo itapunguza gharama kwa wagonjwa hao wanaolazimika kutafuta huduma hizo katika kaunti jirani ya Mombasa.

“Nafikiri si kitambo watu wetu watapumzika kwenda kutafuta huduma hizi katika kaunti nyingine kwa sababu huduma hizo zote zitakuwa zinapatikana pale na kutakuwa na wahudumu wa kutosha ili kuhakikisha kila kitu kinafanyika inavyofaa,” akasema Bw Hamisi.

Mbali na hayo, mkurugenzi huyo amebainisha kwamba serikali ya Kilifi chini ya uongozi wa gavana Mung’aro imelipatia kipaumbele swala la afya ili kuhakikisha kila mkazi wa kaunti hiyo anapata huduma bora za afya.

  • Tags

You can share this post!

Mauzo: Ngamia wachelewesha meli kuondoka bandarini Lamu

Indonesia yaharamisha ngono nje ya ndoa

T L