Habari Mseto

Kaunti ya Lamu yafadhili elimu ya wanafunzi 800

February 20th, 2019 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

JUMLA ya wanafunzi 801 wamefadhiliwa na serikali ya Kaunti ya Lamu katika harakati zake za kusaidia kuafikiwa kwa mpango wa serikali ya kitaifa wa asilimia 100 ya wanafunzi wa shule za msingi wanaojiunga na sekondari nchini.

Gavana wa Lamu, Fahim Twaha, anasema serikali yake imejitolea kikamilifu ili kuona kwama mpango huo unaafikiwa vyema Lamu.

Katika hotuba yake ya tathmini ya hali ilivyo kaunti ya Lamu aliyoitoa kwenye bunge la kaunti ya Lamu Jumatano, Bw Twaha alisema ili kuinua kiwango cha elimu kote Lamu, Kaunti imeafikia kuongeza mgao wa elimu wa kila mwaka kutoka Sh 60 milioni hadi Sh 127 milioni.

Mapema mwaka huu, serikali ya kaunti ilikuwa imetangaza ufadhili wa wanafunzi wote waliozoa alama 300 na zaidi kwenye mtihani wa kitaifa kwa darasa la nane (KCPE) ili kujiunga na shule za sekondari.

Bw Twaha alisema wanafunzi hao ni miongoni mwa 801 ambao tayari kaunti imehakikisha wamejiunga na shule za upili.

“Tunafurahia kwamba tumepiga hatua nzuri katika maendeleo ya elimu eneo hili. Kaunti imejitahidi na kuwafadhili wanafunzi wapatao 801 ambao tayari wamejiunga na shule za sekopndari eneo hili. Haya yote yameafikiwa hasa baada ya utawala wangu kuongeza mgao wa kila mwaka wa basari kutoka Sh 60 milioni hadi Sh 127 milioni. Tutaendelea kujitolea ili kuona kwamba elimu inaboreshwa eneo hili,” akasema Bw Twaha.

Alisema kaunti pia iko mbioni kutekeleza ujenzi na uboreshaji wa miundomsingi kwenye shule za chekechea na vyuo anuwai (TVET) ili kuona kwamba masomo kwenye vituo hivyo yanaendelea bila kutatizwa.

Alisema kaunti tayari imeajiri walimu wa kutosha wa chekechea.

Gavana huyo pia alisema ili kuinua hali ya maisha kwa vijana wa Lamu, kaunti pia imejitolea kuwafadhili vijana 100 kwa kila wadi kati ya wadi zote 10 za Lamu katika mafunzio ya kuendesha magari.

“Tutawapeleka kwenye vyuo vya kujifunza udereva. Punde watakapohitimu wataweza kujitafutia kazi kwenye kampuni mbalimbali na kuendeleza maisha yao,” akasema Bw Twaha.