NA VALENTINE OBARA
GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, amedokeza mipango ya kaunti hiyo kubuni sheria mpya itakayoisaidia kunufaika kutokana na makongamano mengi yanayoandaliwa hotelini.
Akizungumza Jumatatu wakati wa warsha ya viongozi wa mashtaka, Bw Nassir alisema kaunti inalenga kukuza mbinu ya kuvutia watalii kupitia kwa warsha na mikutano.
“Tunataka kuwa na sheria ndogo ya kaunti ambayo itahakikisha watu wanapokuja kwa mikutano kama hii wanatumia pesa zao ndani ya kaunti hii,” akasema.
Tofauti na miaka iliyopita ambapo sekta ya utalii haikuwa na shughuli nyingi mwanzoni mwa mwaka, hoteli za ukanda wa Pwani zimenufaika mwaka huu kwani kumekuwa na mikutano mingi ya idara za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Hali hii imeendeleza mavuno yaliyokusanywa katika sekta hiyo mwishoni mwa mwaka uliopita ambapo idadi ya watalii iliongezeka ikilinganishwa na miaka ya awali iliyokumbwa na vikwazo vya janga la Covid-19.
Bw Nassir ambaye alikuwa ameandamana na Rais William Ruto katika warsha hiyo, alimwomba kuwa serikali ya kitaifa pia ichangie katika kukuza mbinu hiyo ya utalii.
Wawili hao baadaye walihudhuria pamoja warsha ya wabunge wa taifa iliyoandaliwa na Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA).
Wabunge takriban 300 wamekuwa Mombasa tangu wiki iliyopita ambapo walikuwa na mkutano wa mafunzo kuhusu shughuli za bungeni.
Katika kongamano la viongozi wa mashtaka, Bw Nassir alieleza kuhusu umuhimu wa asasi za kisheria kuungana ili kukabiliana na uhalifu wa kimataifa.
Bw Nassir alisema Kaunti ya Mombasa ni mojawapo ya zile zinazoathirika na aina hiyo ya uhalifu unaojumuisha ulanguzi wa mihadarati, uhamishaji wa watu kiharamu, ugaidi, miongoni mwa mengine.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji, alisema juhudi za kukabiliana na uhalifu huo zitafanikiwa kupitia kwa ushirikiano wa asasi za kisheria kimataifa.