Habari Mseto

Kaunti ya Nairobi yazidi kutwaa nafasi za maegesho zilizonyakuliwa

December 17th, 2018 1 min read

NA COLLINS OMULO

SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi sasa imeimarisha juhudi za kutwaa ardhi inayomilikiwa na wanyakuzi, ili kuongeza nafasi ya maegesho ya magari jijini.

Mkurugenzi wa maegesho katika kaunti hiyo Bw Tom Tinega amesema kuwa idara hiyo inalenga maeneo 50 ya maegesho yaliyonyakuliwa katikati ya jiji ili kusuluhisha tatizo la uhaba wa maegesho.

Bw Tinega alisema kuwa maeneo matatu likiwemo eneo la Jumba la Nyayo lenye uwezo wa kuegeshea magari 200 tayari yametwaliwa.

Alisema eneo hilo lilikuwa limenyakuliwa na mwekezaji wa kibinafsi ambaye alikuwa ameligeuza kuwa mali yake huku lingine lililoko barabara ya Haille Selassie mnyakuzi akiwa tayari ameweka mashine za kulipisha ada ya maegesho.

“Kufikia sasa serikali ya kaunti imetwaa maeneo matatu ya uegeshaji katikati ya jiji yenye nafasi 200 za kuegesha magari katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita,” akasema jana.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa operesheni hiyo itazidishwa katika kipindi cha wiki zijazo kabla ya kuendelezwa nje ya jiji na kuingia mitaani.

Alisema operesheni hiyo inalenga kuwapa wenye magari nafasi zaidi za uegeshaji kabla ya kuzinduliwa kwa huduma mpya ya mabasi inayolenga kupunguza msongamano katikati ya jiji.

“Tunataka kuwaonya wanyakuzi kuwa hatutawapa fursa ya kuvunja sheria. Gavana Mike Sonko ametoa ilani kwa uongozi wake kumaliza unyakuzi wa ardhi,” akasema.

Nafasi zote za uegeshaji katika jiji la Nairobi kijumla ni 14,864 ambapo 3,941 ziko barabarani, na kuwakilisha asilimia 26.5 ya zote. Zile ambazo haziko barabarani ni 3,834 huku 7,089 zikiwa kwenye majengo.

10,399 kati yazo zinatumika kwa uegeshaji wa kila siku na wamiliki wa tiketi za mwaka mzima.

Kumekuwa na mipango ya kuongeza nafasi hizi kufika 20,000 ili kuongezea pato la kaunti ambalo limekuwa likididimia tangu 2013 na kufikia Sh3 bilioni kwa mwaka.