Habari Mseto

Kaunti ya Nyeri yatenga kipande cha ardhi kufanyia miradi kama njia ya kukumbuka wapiganiaji uhuru

February 19th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI ya Kaunti ya Nyeri imetenga kipande cha ardhi ukubwa wa ekari moja kufanya miradi ya maendeleo yatakayohusishwa na mashujaa waliopigania uhuru wa Kenya kupitia vuguvugu la Maumau.

Gavana Mutahi Kahiga amesema kipande hicho cha ardhi kitatumika kujenga shule na makavazi, kwa kile anataja kama kuwakumbuka kwa njia ya heshima.

“Waliopigania uhuru wa Kenya ni mashujaa; tusipofanya maendeleo yanayohusishwa nao vizazi vyetu vijavyo havitawajua siku za usoni. Watakuwa wakiwasoma kwenye vitabu vya historia,” Kahiga akasema.

Akizungumza Jumanne katika hafla ya ukumbusho wa mpiganiaji uhuru Dedan Kimathi eneo la Nyeri, gavana huyo aliihimiza serikali kuu kuunga mkono na kushirikiana kwa karibu na serikali ya kaunti hiyo katika azma yake kukumbuka mashujaa.

“Tunaomba serikali kuu itutengee ekari tano zaidi,” akasema.

Dedan Kimathi Wa Waciuri, alikuwa ‘mwanajeshi’ na kiongozi wa vuguvugu la Maumau ambalo lilisaidia kupigania uhuru wa Kenya kwa kuondoa serikali ya mkoloni.

Maumau ni jina lenye asili ya Agikuyu maana yake kwa kina ni ‘Ondoka Ondoka’ na Kimathi aliongoza mashujaa wenza kufurusha wakoloni miaka ya hamsini.

Operesheni ya mashujaa hao iliendeshwa kwenye misitu, na mnamo 1956 alipigwa risasi na kukamatwa ambapo alifikishwa kortini, chini ya mahakama za kikoloni, akafunguliwa mashtaka ya kumiliki silaha hatari.

Tangu afariki, alizikwa mahali pasipojulikana na kufikia sasa mabaki ya mwili wake hayajawahi kuonekana.