Kaunti yaanza kuwalipa fidia wakazi wa Buxton

Kaunti yaanza kuwalipa fidia wakazi wa Buxton

Na SIAGO CECE

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imeanza kuwalipa pesa wakazi wa Buxton ili kuwasaidia kuhamia kwingineko baada ya nyumba zao kubomolewa kutoa nafasi ya ujenzi wa nyumba za kisasa.

Walipewa hundi ya thamani za Sh240,000 za kuwawezesha kukodisha nyumba sehemu mbadala kuruhusu ujenzi wa nyumba mpya zitakazogharimu Sh6 bilioni katika mtaa huo.

Hii ni baada ya mahakama ya mazingira na ardhi Mombasa kutupilia mbali ombi la baadhi ya wakazi hao waliotaka mradi huo wa ujenzi wa nyumba usitishwe

Aidha, shughuli za ubomoaji wa nyumba mtaani Buxton zilianza Ijumaa hatua iliyosababisha baadhi ya wakazi kuanza kuhama.

Zaidi ya nyumba 500 zinatarajiwa kubomolewa na zingine 1860 kujengwa kutumia mitindo na muundo wa kisasa.

Mradi huo wa nyumba za gharama nafuu unalenga kuwawezesha wanachi kuwa wamiliki nyumba.

Hii ni kutokana na ushirikiano kati ya mwekezaji wa kibinafsi Suleiman Shahbal na Gavana wa Mombasa Hassan Joho kupitia serikali ya kaunti.

Ubomoaji huo unajiri baada ya serikali ya kaunti ya Mombasa kuwapa wamiliki wa nyumba hizo notisi waondoke

Joseph Murage, ambaye amekuwa mpangaji kwa miaka 20 alisema pesa hizo zitamfaa kukodisha nyumba kwingineko akisubiri ujenzi wa nyumba hizo ukamilike.

“Nyumba zilikuwa zimechakaa kwa sababu ni za zamani sana. Natumai sasa, sitakuwa tu mmiliki wa nyumba, lakini pia nitaishi katika nyumba nzuri, “akasema alipokuwa akipokea hundi yake.

Wale waliopokea hundi walihitajika kutia saini mikataba miwili, moja ikiwa ya kuhama na nyingine ya umiliki wa nyumbani mpya.

Wakazi hao wanatarajiwa kupokea fidia ya Sh300, 000 lakini wale wanaopenda kumiliki nyumba mpya baada ya ujenzi wanatarajiwa kulipa amana ya Sh60,000.

Afisa Mkuu wa Ardhi na Upangaji wa Kaunti ya Mombasa Dkt June Mwajuma alisema kuwa mara tu ujenzi utakapoanza, itachukua muda wa miezi 12 kwa awamu ya kwanza kumalizika.

“Mradi unatarajiwa kuanza na awamu ya kwanza kukamilika kwa miezi 12, “alisema wakati wa zoezi la utoaji wa hundi hizo kwa wakazi hao.

Pia, alisema, huu ni mpango wa gharama nafuu wa nyumba ambao wakazi watakuwa na umiliki kamili wa nyumba hizo.

Huku shughulli hio ikiendelea, baadhi ya wapangaji waliopata hundi hizo wametoa shukrani kwa kaunti ya Mombasa.

Wiki iliyopita, mahakama ya Mazingira na ardhi ilitupilia mbali kesi ya kupinga utekelezaji wa mradi wa nyumba za gharama nafuu wa Sh6 bilioni na serikali ya kaunti ya Mombasa, kwa kushirikiana mwekezaji wa kibinafsi.

You can share this post!

Uhuru aamuru ardhi ya KDF irejeshewe jamii ya Samburu

DINI: Tuwe kama bundi; tuutumie usiku ‘kuona’ yale...