Habari Mseto

Kaunti yaelimisha maafisa kutatua kesi za mashamba

July 21st, 2019 1 min read

Na ERIC MATARA

SERIKALI ya Kaunti ya Nakuru imeamua kutoa mafunzo kwa maafisa ili wawe wakitatua mizozo ya umiliki wa mashamba, kama mbinu ya kupunguza idadi ya kesi za mashamba ambazo zinafikishwa kortini.

Gavana Lee Kinyanjui jana alisema kuwa kesi nyingi ambazo zinapelekwa kortini zinaweza kusuluhishwa nje ya korti,.

Alisema hatua hiyo itasaidia serikali yake kuendelea kutoa hati za umiliki kwa watu wengi na kwa haraka.

“Kaunti imeanza kutoa mafunzo kwa maafisa wetu na wale wa serikali kuu kuhusu mbinu mbadala za kusuluhisha kesi za mashamba, ili tuharakishe zoezi hili,” Gavana Kinyanjui akasema.

Gavana huyo aliwaambia wakazi kuwa hati za umiliki zitakuwa za manufaa kwao, akisema hazitaonyesha tu kuwa mtu anamiliki ardhi, bali pia zitawawezesha wakazi kujikuza kiuchumi kwani wanaweza kuzitumia kupata mikopo na kufanyia biashara ama kilimo.

Serikali ya kaunti hiyo pamoja na Serikali Kuu zimekuwa zikishirikiana kuendesha zoezi hilo la kutoa hati za umiliki wa mashamba kwa wakazi.

Kulingana na takwimu katika mahakama za kaunti hiyo, hata hivyo, nusu ya kesi zilizoko kortini zinahusiana na mashamba, hali ambayo Gavana Kinyanjui anasema inatishia kutofanikisha zoezi la utoaji hati hizo.