Habari Mseto

Kaunti yafungua soko la mifugo la Nagele

November 22nd, 2019 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imefungua rasmi soko la mifugo lililojengwa eneo la Nagele, tarafa ya Witu kwa kiasi cha Sh18 milioni.

Ufunguzi wa soko hilo la Nagele ni afueni kwa wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo kote Lamu ambao kwa miaka mingi wamelazimika kutembea mwendo mrefu hadi mjini Garsen, Kaunti ya Tana River ili kutafuta soko la mifugo yao.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa soko hilo kijijini Nagele, Afisa Msimamizi wa Idara ya Mifugo na Vyama vya Ushirika wa serikali ya Kaunti ya Lamu, Gichohi Mathenge, alisema soko hilo linatarajiwa kuipa hadi Sh20 milioni kwa mwaka kutokana na mapato ya kodi yanayotokana na uuzaji na ununuzi wa mifugo sokoni humo.

Bw Mathenge alisema matarajio yao ni kwamba soko hilo la mifugo liinue wafugaji na hata wafanyabiashara wa mifugo kote Lamu.

Aliwataka wananchi kushirikiana vilivyo na utawala wa kaunti ili kufaulisha mipango yote ambayo kaunti iko nayo.

“Tunafurahia kufungua rasmi soko la Mifugo la Nagele. Soko lenyewe lilijengwa kwa kiasi cha Sh18.2 milioni. Kama kaunti, tunatarajia soko hili kuinua hali ya maisha kwa wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo ambao watapumzika safari ndefu kutoka Lamu na wanyama wao hadi Tana River ili kutafuta soko la mifugo. Kaunti pia inatarajia kuongeza mapato ya kodi kutokana na ununuzi na uuzaji mifugo hapa Nagele,” akasema Bw Mathenge.

Naye Afisa wa Mipango na Makadirio katika Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Peter Arucho alitaja uzinduzi wa soko la Nagele kujiri kwa wakati ufaao.

Bw Aruchpo alisema soko hilo litasaidia kuinua uchumi na hali ya maisha ya wafugaji na wanabiashara wengi wa Lamu ambao wamekuwa wakikumbwa na matatizo ya tangu jadi ya kusafirisha mifugo wao hadi kwenye soko la Garsen, Kaunti jirani ya Tana River.

“Natarajia kwamba soko la Nagele litapunguza gharama za wafugaji na wanabiashara wa mifugo kusafirisha wanyama wao hadi Garsen ambako ni mbali kutoka Lamu,” akasema Bw Arucho.

Kwa upande wake, Afisa wa Bodi ya Mikopo ya Kilimo (AFC), tawi la Lamu, John Ochanda aliwahimiza wafugaji kuunda vikundi na kujichukulia mikopo itakayosaidia kuinua maisha yao.