Habari Mseto

Kaunti yalaumiwa kwa mgao mdogo wa kupiga vita malaria

September 3rd, 2019 1 min read

Na FLORAH KOECH

SERIKALI ya Kaunti ya Baringo imeshutumiwa kwa kutenga Sh2 milioni kwa ajili ya kupambana na malaria licha ya wakazi wa eneo hilo kukabiliwa na mkurupuko wa maradhi hayo mara kwa mara.

Watu zaidi ya 30 wamefariki katika Kaunti ya Baringo kutokana na malaria katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Watu 10 waliaga dunia wiki mbili zilizopita kufuatia mkurupuko wa malaria eneobunge la Tiaty.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa serikali ya Kaunti ya Baringo ilitengea malaria Sh2 milioni pekee katika mwaka wa 2019/2020. Mwaka uliopita wa 2018/2019, kaunti haikutengea maradhi hayo fedha zozote.

Watu 20 walipofariki mnamo 2017, serikali ya kaunti iliahidi kujenga vituo vya afya na kununua magari ya ambulansi. Afisa wa Matibabu wa Baringo, Gideon Toromo alisema serikali ya kaunti ilianza kutenga fedha za kuzuia na kukabiliana na ugonjwa wa malaria mwaka huu.

“Tangu kutokea kwa mkurupuko wa malaria 2017, hatujawahi kutenga fedha kwa ajili ya ugonjwa huo. Lakini mwaka huu tumeamua kutenga Sh2 milioni,” akasema Dkt Toromo. Afisa wa huduma za afya alisema fedha zinazotengewa idara ya afya ni kidogo mno.

“Kukabiliana na malaria katika eneo hili tunahitaji zaidi ya Sh20 milioni kila mwaka. Hata sasa hatuna fedha za kuendesha shughuli katika wizara ya afya. Hatuna fedha za kukarabati ambulansi,” akasema.

Alisema kaunti iliweza kukabiliana na mkurupuko wa malaria wiki chache zilizopita baada ya kupokea msaada kutoka kwa wahisani.

“Serikali ya kaunti imetuma maafisa wa afya katika vijiji vyote vilivyoathiriwa ili kukabiliana na maradhi hayo. Tunashirikiana na Kanisa Katoliki la Barpello,” alisema.