Habari Mseto

Kaunti yapanda miti kwa ardhi iliyotumika kama dampo Nyali

June 8th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

SERIKALI ya kaunti ya Mombasa imeanza kupanda miti katika sehemu iliyokuwa jaa la VOK eneo la Nyali.

Kipande hicho cha ardhi yenye ukubwa wa hekari 22 ambacho kinamilikiwa na Shirika la Habari Nchini (KBC), kilitumika kama jaa kwa miaka mingi hali iliyoweka afya za wakazi wa eneo hilo hatarani.

Hali hiyo iliwafanya wataalamu wa mazingira kuingilia kati na kuagiza jaa hilo ambalo lilikuwa linapakana na makazi ya watu kufungwa.

Serikali ya Kaunti ya Mombasa imechukua hatua ya kupanda miti katika sehemu iliyotumika kama jaa la VOK, Nyali. Picha/ Mishi Gongo

Mwaka 2019 serikali ya kaunti hiyo iliahidi kuwa kufikia Juni 2020 jaa hilo litakuwa limefungwa na huduma kama hizo ziwe Mwakirunge.

Kulingana na waziri wa mazingira katika kaunti hiyo Dkt Godfrey Nato, taka katika jaa hilo ziliondolewa mwanzoni mwa Mei 2020.

Shughuli za upanzi wa miti katika sehemu hiyo zilianza Ijumaa wiki jana ambapo dunia ilikuwa inaadhimisha Siku ya Mazingira.

“Jaa lilikuwa linachafua mazingira. Tumeamua kupanda miti ili kuboresha mazingira. Kabla kupanda miti tulifanya ardhi kuwa tambarare kisha kujaza mchanga,” akasema Dkt Nato.

Baadhi ya wafanyakazi wa serikali ya Kaunti ya Mombasa wapanda miti sehemu iliyotumika kama jaa la VOK, Nyali. Picha/ Mishi Gongo

Alisema walifaulu kufunga jaa la Kibarani na kugeuza sehemu hiyo kuwa bustani maridadi.

Jaa la Kibarani lilikuwa na zaidi ya miaka 50.

Waziri huyo alisema wanapangia kuwa na sehemu moja pekee ya kutupa taka ili kuhifadhi mazingira.

Kulingana na umoja wa Mataifa kaunti ya Mombasa hukusanya takriban tani 900 za taka kila uchao.

“Tunawaomba wakazi kutusaidia katika kudumisha mazingira. Takriban asilimia 80 ya nyumba ziko na watu wa kukusanya taka, hivyo tujitahidi kuweka jiji letu kuwa safi. Kaunti inauwezo wa kukusanya asilimia 47 pekee,”akasema Dkt Nato.